Nilikuwa nina mahusiano yangu ya muda mrefu, lakini nilikuwa nina migogoro ya mara kwa mara na huyo mwanamume. Nikakutana na mwingine aliyeonyesha nia na niliona ana sifa ninazozitaka nikakubali kuwa naye.
Kabla sijakubali nilitaka kujua kuhusu uhusiano wake uliopita japo kwa ufupi, alinielewesha kuwa waliachana kwa sababu ilishindikana kuendelea, nilimuelewa kwani sikutaka kuhoji zaidi, maana siyo sehemu ya mahusiano yetu.
Dah! Kumbe nilikosea, kwani nilikuja kugundua baadaye huyu mwanamume hajaachana na huyo mpenzi wake, waligombana na kutengana kwa muda, hivyo wamemaliza tofauti zao na wamerudiana.
Roho inaniuma sana, kwani hata mimi angeniacha na maisha yangu ningemaliza tofauti na mtu wangu, ila alinihakikishia usalama wa moyo wangu.
Nisaidie ushauri nimfanye nini ili asirudie kuwafanyia wanawake wengine mambo kama aliyonifanyia mimi.
Kukumbana na hali ambapo mpenzi wako amerudi kwa mwanamke wake wa zamani ni tukio gumu na la kuhuzunisha.
Katika maisha, mara nyingi tunakutana na changamoto ambazo zinatufanya tuhisi huzuni, mshangao na hata hasira.
Hali hii inaweza kukuganda katika mawazo yako, ikikuacha na maswali mengi kuhusu thamani yako binafsi na mahusiano yaliyowahi kuwepo. Ingawa ni rahisi kujisikia kushindwa na kukatishwa tamaa, kuna njia kadhaa za kukabiliana na hali hii, badala ya kufikiria kumuadhibu.
Kwanza kabisa, ni muhimu kukubali hisia zako. Unaweza kujisikia huzuni, hasira, au hata wasiwasi kutokana na mabadiliko haya. Kukubaliana na hisia hizi ni sehemu ya mchakato wa kuponya. Pata muda wa kutafakari suala hilo na kukubaliana nalo, hii itakusaidia kuendelea na maisha mengine kuliko kuendelea kumlaumu au kumfikiria mtu aliyeamua kuishi maisha yake na kuufikiria zaidi moyo wake unataka nini.
Hata hivyo, usiruhusu hisia zako zikufunge kwenye dimbwi la huzuni. Tafuta njia za kuusafirisha uelekeo wa hisia zako, kama vile kuzungumza na rafiki yako wa karibu kuhusu suala hilo ili upate amani.
Hakuna jambo lisilo na mafunzo, hivyo tafakari pia nini umejifunza kutokana na uhusiano huo. Kila uhusiano una thamani yake, na inaweza kuwa ni fursa ya kukua. Tafakari kuhusu mambo uliyofanya vizuri na yale unayoweza kuboresha katika siku zijazo. Hii itakusaidia kuwa na mtazamo chanya na kukuandaa kwa uhusiano mwingine katika siku zijazo, kwani lazima maisha yaendelee.
Usisahau unastahili kupata upendo na heshima, uhusiano wa kweli unahitaji pande zote mbili kuheshimiana. Ikiwa mpenzi wako aliamua kurudi kwa mwanamke wake wa zamani, hiyo ni ishara kwamba huenda hata yeye hakujihisi thabiti kwenye uhusiano wenu. Hii inamaanisha kwamba ulifanya vizuri katika kumfanya ajiangalie, lakini pengine hakuwa tayari kuchukua hatua muhimu za kuweka uhusiano wenu imara.
Usikubali kujisikia vibaya au kutopenda tena, unastahili mtu ambaye atakuthamini na kukujali.
Pia, jikumbushe kuhusu malengo yako binafsi na mambo unayopenda kufanya. Hii ni fursa nzuri ya kujijenga na kujitafutia mambo mapya.
Fanya mambo ambayo yanakufurahisha na kukupa furaha. Kuungana na marafiki, kujihusisha katika shughuli za kijamii, au hata kujifunza ujuzi mpya ni njia bora ya kujitenga na huzuni iliyokusumbua.
Usikubali kuingia kwenye malumbano na mwanamume aliyekuacha wala kufuatilia maisha yake, kwani hiyo itampa nafasi ya kuwachezea akili wewe na huyo Ex wake. Atakuwa anakudanganya kwa hili na lile na mwenzako akimdanganya pia, hiyo itakuwa mbaya zaidi ya hii ya sasa.
Kusonga mbele kwa furaha, kujijali, kujipenda, kutosikiliza maneno ya waja ndiyo dawa pekee.