Viongozi wa dini, Serikali wasisitiza amani na utulivu

Pwani. Watanzania wametakiwa kulinda, kutunza amani na utulivu hasa kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika mwakani.

Viongozi wa dini ya Kiislamu wametoa rai hiyo kwenye kongamano na dua maalumu ya kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan iliyoandaliwa na mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega, kwa ushirikiano na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) wilayani humo.

Dua hiyo iliyofanyika jana Desemba 14, 2024 katika viwanja vya Shule ya Msingi Mkuranga ilitanguliwa na Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika asubuhi yaliyowakutanisha masheikh wakiwemo wa mikoa ya Arusha, Kigoma, Kagera, Dar es Salaam na Pwani.

Maulid hayo yalibeba kaulimbiu ya ‘Tulinde maadili yetu na amani yetu kwa masilahi ya Taifa letu’. 

Watanzania wamesisitiziwa kuitunza na kuimarisha amani iliyopo ili kuunga mkono jitihada za Rais Samia aliye mstari wa mbele kuihubiri, akikemea mmomonyoko wa maadili akiwataka viongozi wa dini kuungana na Serikali kusimamia suala hilo.

Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Shaaban Juma amesema kongamano lililoambatana na dua lina tafsiri nyingi, ikiwemo kutoa maelezo au ishara kwamba amani imetawala.

“Nchi isiyokuwa na amani, mkusanyiko kama huu wa kumswalia Mtume Muhammad (S.A.W) kumuombea dua Rais wetu na Taifa kwa ujumla inakuwa ni vigumu, lakini Tanzania tumebarikiwa kuwa na amani tuilinde na kuitunza.”

“Mali au fedha unaweza ukazificha mfukoni au mahali pengine, lakini binadamu utamficha wapi asione na shari au dhuluma? Amani ndiyo kila kitu ndugu zangu, tuitunze, namshukuru Ulega na wenzake kufanya tukio kama hili, muda huu tungekuwa tumelala lakini tupo hapa sasa hivi (saa tano usiku)” amesema.

Mjumbe wa Baraza la Ulamaa la Bakwata, Sheikh Himid Jongo kwa niaba ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, amempongeza Ulega kwa kuandaa tukio hilo, akisema Watanzania wamepata fursa ya kumuombea Rais Samia na Taifa kwa ujumla.

Pia amewashukuru mawaziri na wananchi waliojumuika katika tukio hilo.

Sheikh Jongo alimuomba Ulega kushughulikia changamoto ya ufinyu wa barabara eneo la Mto Mzinga, Mbagala akisema limekuwa kero kwa muda mrefu.

“Mama (Rais Samia) amekupa jembe (Waziri wa Ujenzi) basi ulime kweli,” amesema.

Ulega amekuwa akiandaa maulid kila mwaka, huku 2024 yakivuta idadi kubwa ya wahudhuriaji.

Miongoni mwa mawaziri waliokuwapo ni Jumaa Aweso (Waziri wa Maji) na Ridhiwani Kikwete (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu). Wawili hawa walikuwa kivutio kwa kuimba Qaswida kwa umahiri mkubwa.

Wengine ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deo Ndenjembi na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa. Pia walikuwepo mameya, wakurugenzi na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.

Ulega amemshukuru Mungu na Rais Samia kwa kuendelea kumuamini, akiahidi kutomuangusha katika utekelezaji wa majukumu yake mapya ya sekta ya ujenzi.

“Hadhara hii imekuwa kubwa, nimshukuru Mungu, shukrani yangu ya pili ni kwa Rais Samia kwa kuendelea kuniamini kwa kunipa nafasi ya kumsaidia, namuahidi kuendelea kufanya kazi kwa moyo wangu usiku na mchana ili kulisaidia Taifa,” amesema.

Amewashukuru waliohudhuria, wakiwemo masheikh kutoka kata zote 25 za Mkuranga.

“Umati huu umetoka katika vijiji vyote vya kata 25 za Wilaya ya Mkuranga, hadhara kama hizi, tumejiwekea malengo pia ya kuboresha huduma za jamii zetu,” amesema.

Mkazi wa Kata ya Kisiju, Mohamed Mperi amesema: “Hili ni tukio adhimu linalokutanisha wananchi mbalimbali kwa ajili ya dua maalumu. Tukio hili linasaidia kujuana, kukutana na kutoa mafundisho ya upendo wa watu kupendana na kubadilishana mawazo,” amesema.

Kunenge amesema Rais Samia amefanikiwa kuweka mazingira mazuri ya amani katika maeneo mbalimbali, ndiyo maana tukio hilo limefanikiwa.

Related Posts