Hiki ni kipindi cha mapumziko kwa wanafunzi wa shule za awali, msingi na sekondari na ndicho kipindi kinachoambatana na sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Licha ya kuwa muda wa kupumzika, wazazi wanapaswa kuwahimiza watoto wao kujiandaa kwa mwaka mpya wa masomo utakaoanza Januari, 2025.
Kwa baadhi ya familia, likizo hutumika kuwashirikisha watoto kwenye kazi mbalimbali kama kilimo, kuhudumia mifugo, au biashara ndogo ndogo ili kusaidia kipato cha familia. Wengine hutumia muda mwingi kuangalia runinga na kucheza michezo ya video.
Ingawa si vibaya, lakini wazazi wanapaswa kuwa waangalifu kwa kuhakikisha maudhui yanayotazamwa yanafaa na hayaathiri maadili ya watoto.
Niliwahi kusoma mahali, kuwa wazazi si walimu, lakini wanapaswa kupangilia likizo za watoto wao.
Wanasema sababu kubwa ni kuwa, likizo inapaswa kuwa na ratiba inayowawezesha watoto kupumzika, kujifunza kwa kiwango kinachofaa na kujiburudisha pia.
Ingawa si lazima mtoto apelekwe kwenye masomo ya ziada, wazazi wanapaswa kuwasaidia watoto kukumbuka masomo ya darasani kwa njia zisizobana.
Hii inaweza kujumuisha umuhimu wa wao kutembelea maktaba, kusoma vitabu vya kujiburudisha na kielimu au kutazama video zenye maudhui mazuri yanayohusiana na masomo yao.
Na wazazi mnapaswa kukumbuka kuwa tabia ya kutembelea maktaba huchochea watoto kupenda kujisomea, hili hata ninyi baadhi yenu mlilifanya wakati mnakua.
Hivyo ni vema kuwarithisha watoto wenu utamaduni huo kwa kuwahimiza kutembelea maktaba kwenda kuperuzi mambo mengi.
Hii ni hatua muhimu kwa maendeleo ya mwanao kuendelea kukuza ufahamu na ujuzi wa mambo kadhaa anayosoma akiwa shuleni, maktaba atakwenda kuyafanyia rejea, hivyo akili yake itaendelea kuchangamka na akirejea shuleni mwakani, bado akili itakuwa imechangamka haijalala.
Pia huwasaidia kujenga msingi mzuri wa kitaaluma na utamaduni wa kujisomea hata baada ya shule.
Lakini wazazi wakumbuke kuwa kipindi hiki ni fursa kwao kuwashirikisha watoto kwenye shughuli za familia, kama vile kuwatembelea ndugu na jamaa ili kubadilisha mazingira. Shughuli hizi huwasaidia watoto kuona mambo mapya, kujifunza, na kujenga mahusiano mazuri ya kijamii.
Aidha, wazazi wanaweza kutumia muda huu kujadili na watoto mustakabali wa familia yao na kufanya tathmini ya matokeo ya mitihani yao. Hii inatoa nafasi ya kuwapongeza kwa mafanikio na kuwaelekeza jinsi ya kuboresha pale walipopatwa na na changamoto na wakajikuta wakifanya vibaya kwenye mitihani yao ya mwisho.
Ila jambo lingine kubwa ni hili la umuhimu wa kupumzika. Hiyo ni sehemu muhimu ya maendeleo ya mtoto.
Likizo inampa mwanafunzi nafasi ya kupumzisha akili na mwili, kumwezesha kuanza muhula mpya wa masomo akiwa na nguvu na ari ya kujifunza zaidi.
Kinyume chake, mzazi anayebana mtoto na kumlazimisha kuendelea na masomo mfululizo anaweza kusababisha uchovu wa akili, hali inayoweza kudumaza uwezo wa mwanafunzi kufikiri na kushindwa kufaulu katika masomo yake.
Hivyo ni vema wazazi mkazingatia kwamba likizo si muda wa kusoma tu, bali pia ni fursa ya kujifunza kwa njia mbadala, kuburudika na kujiandaa kwa masomo yajayo.
Mnashauriwa kuwa sehemu ya safari ya likizo ya watoto wenu, iwasaidie kuendesha maisha yao ya likizo kwa mpangilio mzuri unaolenga kuwajenga kielimu, kiakili na kijamii.
Kwa kufanya hivyo, watoto wanaweza kufurahia likizo na kurejea shuleni wakiwa na ari na nguvu mpya ya kujifunza zaidi.