Uwajibikaji unavyoweza kupandikizwa kwa mtoto

Dar es Salaam. Tafsiri ya kitaalamu inaelezea malezi kuwa ni mchakato wa maandalizi ya mtoto utakaomwezesha kukua, kukubalika na kushiriki katika shughuli za kijamii na kiutamaduni kwa kumlinda, kumjamiisha na kumpatia mahitaji na huduma za msingi.

Mzazi ana nafasi ya pekee katika kumwandalia mtoto hatima ya maisha. Ni mtu anayemtunza, kumhudumia na kumfundisha mtoto mpaka akue. Anaweza kumwambukiza tabia njema au mbaya.

Ni kutokana na nafasi ya muda mwingi wa kuishi na mtoto tangu anapozaliwa, hivyo anakuwa na sifa za kuwa mwandishi wa hatima ya mtoto husika.

Ukosefu wa ajira ni janga linalowakabili vijana wengi duniani, Serikali za mataifa tofauti zimekuwa zikiweka mikakati kadhaa kukabiliana na changamoto hii.

Lakini, inaelezwa kuwa familia ni taasisi ya kwanza kutengeneza mazingira rafiki kwa kijana ama kuajirika au kujiajiri.

Hivi karibuni jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa kitabu kinachozungumzia masuala mbalimbali ya fani ya rasilimali watu cha ‘The Business of The People’ hoja ya malezi mabovu kuchangia baadhi ya vijana kushindwa kuajirika iliibuliwa.

Kitabu hicho kimeandikwa na mtaalam wa masuala ya rasilimali watu, Rhoda Benneth ambacho kimeangazia masuala mbalimbali ikiwemo suala la ajira kwa vijana.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho Mshauri wa Masuala ya Rasilimali watu na Biashara, Kabeho Solo anasema pamoja na sababu nyingine ikiwemo mitaala ya ufundishaji, malezi yasiyomuandaa mtoto kujitambua na kuwajibika ni moja kati ya sababu inayofanya vijana wengi kushindwa kuajirika au kudumu katika ajira zao.

Solo ambaye ana uzoefu wa zaidi ya miaka 40 katika fani ya rasilimali watu anasema kutokana na baadhi ya vijana kutoandaliwa kiuwajibikaji na kujitambua wao ni nani na mchango wao katika jamii na taasisi wanazozifanyia kazi inapelekea kutotenda kazi zao kwa ufanisi unaotakiwa.

Pia inasababisha kutoheshimu wala kuzingatia maadili, miiko na taratibu zinazoendesha taasisi wanazozifanyia kazi jambo linalopelekea hata kusababisha migogoro ya mara kwa mara na waajiri wao.

“Pamoja na kuwa mitaala yetu ina changamoto za hapa na pale lakini suala la malezi ni muhimu kutazamwa na kuzingatiwa kwani ndio msingi wa kumjenga kijana ni namna gani unataka awe hapo baadae”anasema.

Anasema zamani wazazi walikuwa wakizingatia kupandikiza mbegu ya uzalendo na uwajibikaji kwa mtoto tangu akiwa mdogo na ndio maana wengi wao waliweza kudumu katika ajira zao.

“Hiyo ndio maana zamani watu waliweza kudumu kwa miaka mingi katika ajira zao labda ikitokea maslahi hayaridhishi au kutaka kupata changamoto mpya na kujifunza zaidi sehemu nyingine na siyo kwa sababu ya kufukuzwa kutokana na utovu wa nidhamu,”anaeleza

Naibu Mkuu wa Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar upande wa Utawala, Mipango na Fedha, Dk Hamad Saidi anasema hilo linasababisha baadhi ya waajiri kulalamika kuwa imekuwa changamoto kufanya kazi na kizazi cha sasa maarufu kama ‘Gen Z’.

Anasema kutokana na kushindwa kuandaliwa na kulelewa katika uwajibikaji baadhi ya vijana wamekuwa na changamoto za utovu wa nidhamu katika maeneo ya kazi.

Pia baadhi yao kulalamikiwa kutotenda kazi zao kwa ufanisi na kuzingatia zaidi masilahi kuliko ufanyaji kazi.

“Vijana wengi wa sasa wanapenda na kufurahi kupata ajira changamoto inakuja katika ufanyaji kazi pale wanapopatiwa nafasi ya kufanya kazi.

Mwandishi wa vitabu na mtaalam wa masuala ya rasilimali watu Rhoda Benneth anashauri kuwa wazazi wanatakiwa kuwajenga watoto katika ari ya kuwa wawajibikaji na wazalendo tangu wakiwa na umri mdogo.

Anasema hiyo itasaidia kuwaandaa watoto kukuwa na tabia hiyo ya kupenda kutekeleza majukumu yao bila ya kushurutishwa.

Vilevile anasema ofisa rasilimali watu pamoja na viongozi wa taasisi nao wana wajibu katika kumsaidia kijana kwa kumtengenezea na kumuwekea mazingira rafiki yatakayomfanya kufanya kazi zake kwa ufanisi.

“Hivyo ni baadhi ya vitu ambavyo vilinisukuma na kuona kuna haja ya kuandika kitabu kitakachosaidia vijana, waajiri,wazazi na jamii kwa ujumla ili kumsaidia kijana kuwa muajibikaji”anasema.

Namna ya kumuandaa kijana kuwa muajibikaji

Akizungumza na Mwananchi mtaalamu wa malezi kutoka Shirika linaloshughulikia masuala ya watoto na malezi la Bright Jamii Initiative, Irene Fugara anasema kumuandaa mtoto kuja kuwa muajibikaji ni mchakato katika malezi ambao unaweza kuanza kufanyika tangu mtoto akiwa na umri mdogo.

Anasema mchakato huo huanza kwa mzazi mwenyewe kwa kuwa kiigizo chema kwa mtoto unaemlea.

Anasema Watoto hufuata mifano ya wazazi wao, hivyo ni muhimu wazazi kuonyesha tabia za kuwa muajibikaji.

Pia anasema wazazi wanapaswa kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na watoto wao kuhusu umuhimu wa kuchukua majukumu yao kwa makini.

Anasema wanapaswa kuzungumza na mtoto juu ya kwa nini ni muhimu kukamilisha majukumu aliyopatiwa kwa wakati na kuzingatia maelekezo aliyopewa.

Vilevile mzazi anaweza kuwapa watoto kufanya majukumu mbalimbali ya nyumbani kulingana na umri wake ambayo yatamsaidia mtoto kumfundisha mtoto kuwa muajibikaji.

Kazi za nyumbani kama vile kupanga vyombo, kufagia, au kutunza wanyama wa nyumbani zinamfundisha mtoto kuwa na nidhamu na kuwajibika kwa majukumu yake.

“Mtoto anapokamilisha majukumu yake, anapata furaha ya kuona matokeo ya juhudi zake, na hiyo inamfundisha umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na kuwa na dhamira katika kutimiza majukumu yake.”anasema.

Related Posts