Pwani. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango amesema nchi itajikita katika vipaumbele tisa, kwenye awamu ya pili ya Kampeni ya Mtu ni Afya.
Vipaumbele hivyo ni pamoja na namna ya kushughulikia magonjwa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo magonjwa ya mfumo wa hewa.
Kampeni ya Mtu ni Afya iliyotimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1973, imeingia katika awamu ya pili kwa mafanikio mengi, ikiwemo kaya zenye vyoo bora kuongezeka hadi kufikia asilimia 74.8 kutoka chini ya asilimia 20 mwaka 1973.
Akizungumza mkoani Pwani wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni hiyo leo Alhamisi, Mei 9, 2024, Dk Mpango ameziagiza Wizara za Afya na Tamisemi kuhakikisha zinasimamia vipaumbele hivyo.
“Awamu ya pili tutajikita katika kushughulikia mambo tisa ambayo ni ujenzi na matumizi ya vyoo bora shuleni, katika vituo vya afya, njia kuu zote za usafiri na maeneo muhimu yenye mikusanyiko,” amesema.
Ametaja unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni nyakati zote na uondoshaji salama wa taka na maji taka.
Amesema nchi itajikita katika kutibu maji ya kunywa au kutumia vidonge maalum vya kutakasa maji kwa maelekezo ya wataalamu.
“Tutajikita katika kuhakikisha hedhi salama kwa watoto wa kike na huduma za usafi shuleni, usafi katika manispaa na miji pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuzingatia mtindo bora wa maisha, ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza,” amesema na kuongeza;
Ameziagiza Wizara hizo kuhakikisha kampeni zinaambatana na elimu kwa umma kuhusu mabadiliko ya tabianchi ili kupunguza magonjwa ya mfumo wa upumuaji.
“Kampeni za mwanzo tuliweka msisitizo kwa magonjwa yatokanayo na usafi, hamasa kubwa ilitolewa kwa wananchi kuzingatia kanuni ya afya bora na njia mbalimbali zilitumika kuhamasisha masuala ya usafi wa mazingira, sasa hali imebadikika,” amesema Dk Mpango.
Pamoja na hayo, makamu wa Rais amesema kampeni hiyo inajumuisha magonjwa yasiyoambukiza, ambayo takwimu zinaonyesha asilimia 9 ya Watanzania wana ugonjwa wa kisukari huku wagonjwa wanne kati ya 10 wakiwa na shinikizo la juu la damu.
Amesema takwimu hizo ni tofauti na zile za mwaka 1980, zilizoonyesha mmoja kwa 100 kwa kisukari na mmoja kwa 20 shinikizo la damu.
Amesema juhudi zaidi pia zielekezwe katika magonjwa ya kuambukiza kwani athari za joto, zinaenda sambamba na magonjwa ya mfumo wa upumuaji na malaria.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kampeni hiyo imekuwa ikibadilika mwaka hadi mwaka.
“Kampeni hii ikitimiza miaka 50, tunazindua awamu ya pili tukiwa na malengo mahususi ya kutokomeza magonjwa ya mlipuko, pia kupambana na magonjwa yasiyoambukiza,” amesema Ummy.
Ametaja mafanikio mengine ya awamu ya kwanza kuwa ni kuimarika kwa huduma za chanjo ambazo kwa kipindi kirefu zimekuwa ukisimamiwa na wataalamu wa afya mazingira na kupitia mpango huo, nchi imeweza kutokomeza magonjwa kadhaa ikiwemo wa ndui uliokuwa tishio duniani.
Washindi usafi wa mazingira
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy amewatangaza washindi wa mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2023, ambapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimetajwa kuongoza, kikilinganishwa na vyuo vikuu vingine nchini.
Nafasi ya pili imechukuliwa na Chuo cha Sokoine na nafasi ya tatu imechukuliwa na Chuo cha Sayansi na Teknolojia Nelson Mandela.