WAKATI dirisha la usajili likifunguliwa rasmi jana kwa ajili ya klabu kufanya maboresho mbalimbali, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma ‘Maniche’, amesema atazingatia maeneo machache kutokana na mahitaji yao na sio kusajili tu ilimradi.
Maniche amekabidhiwa kikosi hicho baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo raia wa Marekani, Melis Medo kuondoka na kujiunga na ‘Wanankurunkumbi’ Kagera Sugar, ikiwa ni baada tu ya kuiongoza timu hiyo katika michezo minne ya msimu huu.
“Tutaangalia maeneo ya kufanyia marekebisho lakini ukiangalia hali ya timu hadi sasa sio mbaya sana, siwezi kuweka wazi hatutasajili isipokuwa tutazingatia nafasi chache, kikubwa ni kuhakikisha tunalinda kwanza tuliokuwa nao wasiondoke.”
Kocha huyo anayeipambania timu hiyo kurejea tena Ligi Kuu baada ya kushuka msimu uliopita, tangu Medo aondoke tayari ameiongoza katika michezo saba kabla ya ule wa jana na Mbeya Kwanza, akishinda minne, sare miwili na kupoteza mmoja tu.
Michezo aliyoshinda ni (3-0) v Africans Sports, (2-0) v Stand United, (2-1) v TMA, (2-0) v Mbuni na sare ni ya (1-1) v Polisi Tanzania na (2-2) v Biashara United, huku kichapo ni cha bao 1-0, dhidi ya Geita Gold, Uwanja wa Nyankumbu Oktoba 25.