Kauli za Polisi, TRA, mke kuhusu mfanyabiashara Ulomi aliyepotea

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeanza kumtafuta mfanyabiashara Daisle Ulomi aliyetoweka katika mazingira yenye utata, Desemba 11, 2024 akiwa kazini kwake Sinza Kijiweni.

Wakati Polisi likitoa taarifa hiyo, mke wa Ulomi, Elizabeth Munisi akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Desemba 15, 2024 amesema tangu alipotoa taarifa Polisi kuhusu kupotelewa na mume wake Desemba 12, hadi sasa bado wako njiapanda, kwani hawajui aliko.

“Jana (Desemba 14) asubuhi nilipigiwa simu na RPC wa Temeke kuniambia bado hawajamuona na wanaendelea kumtafuta, lakini kwa leo bado hawajanipa mrejesho wowote, nasubiri,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa leo Desemba 15, imesema Ulomi hakurudi nyumbani tangu alipoingia kazi kwake, ikidaiwa siku hiyo alionekana akitoka ofisini Sinza Kijiweni saa sita mchana kuelekea Mbagala, Bandari Kavu.

Katika taarifa hiyo, kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema wakati mfanyabiashara huyo anaondoka inadaiwa alikuwa anakwenda kukagua kontena la bidhaa zake baada ya kuitwa na watu waliodai walikuwa wanashughulikia kulitoa bandarini.

“Jeshi linaendelea na ufuatiliaji wa taarifa hiyo kwa kushirikiana na ndugu ili kujua na kubaini yupo wapi,” inaeleza taarifa.

Kamanda Muliro amesema Desemba 12, katika kituo cha Polisi Chang’ombe ilipokewa taarifa ya kutafutwa na familia yake mfanyabiashara huyo.

“Taarifa hiyo inadai Ulomi alikuwa anatumia usafiri wa pikipiki namba MC 415 DQC aliyokuwa akiendesha mwenyewe. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa kuhusiana na mtu huyo azitoe kwenye mamlaka yoyote ya Serikali iliyo karibu yake,” imeeleza taarifa ya Polisi.

Awali, kupitia mitandao ya kijamii kulisambaa taarifa ikieleza mfanyabiashara huyo alipotea wakati anaelekea Bandari Kavu alikoita na watu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kupitia mtandao wa X (zamani twitter) Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob aliandika akidai mfanyabiashara huyo alikwenda bandari kavu kukagua kontena lake baada ya kuitwa na watu wa TRA kwa ajili ya ukaguzi.

Desemba 14, 2024 TRA kupitia kitengo cha Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano, ilitoa taarifa kujitenga na tukio la kupotea Ulomi.

“TRA inautaarifu umma kuwa, mchakato wa uondoshaji wa mizigo bandarini hufanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu za kiforodha. Kwa mujibu wa kifungu cha 2(1) cha Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki, ni wakala wa forodha peke yake ndiye anayewajibika kusimamia taratibu zote za kiforodha za uondoshaji wa mizigo bandarini kwa niaba ya muagizaji wa mzigo na siyo muagizaji wa mzigo.

“Kwa mujibu wa kumbukumbu zetu, mfanyabiashara, Daisle Simon Ulomi aliichagua kampuni ya wakala wa forodha ya Twende Freight Forwarders Limited kupitia barua yake kwa TRA ya   Desemba 5, 2024 kuwajibika kuondosha mizigo yake bandarini kulingana na taratibu za forodha,” imeeleza taarifa hiyo.

TRA imesema imekuwa ikifanya kazi na wakala wake ambaye bado hajakamilisha taratibu za kiforodha kuondosha mzigo husika na kwamba, TRA haijawahi kumuita wala kufanya naye kazi mfanyabiashara huyo katika ofisi zake kwa jambo lolote.

“Suala la kutoonekana kwa mfanyabiashara huyo ni jambo la kipolisi ambalo TRA haihusiki nalo,” imesema taarifa hiyo.

Related Posts