TANZANIA imeunga mkono ombi la Kenya linalokitaka Chama cha Mbio za Magari Duniani (FIA) kupunguza ada ya kibali cha kuandaa mbio za ubingwa wa Afrika sambamba kuwadhamini madereva wanaoshiriki katika raundi zote za mashindano haya.
Rais wa Chama cha Mbio za Magari Tanzania (AAT), Nizar Jivani alisema ni kweli kuna mchakato wa kuyanusuru mashindano ya mbio za magari ubingwa wa Africa (African Rally Championship) na mazungumzo na FIA bado yanaendelea na majibu yake yatatangazwa hivi karibuni.
“Tuko katika mazungumzo na jibu litapatikana mapema juma hili,”€ alisema Jivani.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Desemba 13 na kusainiwa na Mwenyekit Maina Muturi, Shirikisho la Mbio za Magari la Kenya (KMSF) limepeleka ombi kwa FIA likikitaka chama hicho kuyanusuru mashindano ya mbio za magari ubingwa wa Afrika likidai yanaelekea kufa kutokana na gharama kubwa ya ushiriki pamoja na kukosa udhamini maridhawa.
KMSF imetoa mfano kwamba kwa mwaka huu ni dereva mmoja tu Karan Patel ndiye aliyeshiriki mashindano ya ubingwa wa Afrika (ARC) hali ambayo shirikisho hilo limedai ni ishara kuwa, michuano hiyo inaelekea kufa.
Kutoka na hali hii, KMSF imeongeza kwa kusema nchi za Tanzania na Kenya ziliyafuta mashindano ya mwaka huu ya ARC kutokana na kutokuwepo kwa udhamini maridhawa.
Hivyo ili kuyanusuru, KMSF imeiomba FIA kupunguza ada ya kibali cha kufanya mashindano ya ARC, pia kukiomba chama hicho kudhamini madereva wawili kutoka Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda na Zambia, zilizo ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ili waweze kushiriki raundi zote za ubingwa wa Afrika.
Kwa miaka mingi raundi za mbio za magari ubingwa wa magari wa Afrika zimekuwa zikifanyika katika nchi nane za Afrika, lakini miaka ya karibuni baadhi ya nchi zimejitoa katika mashindano haya kutokana na kuyumba kiuchumi.
Kabla ya mtikisiko wa uchumi duniani ambao pia umeiathiri Tanzania, madereva wa Tanzania wamekuwa wakishiriki mara kwa mara katika mbio za ARC nje ya nchi, lakini wengi wameshindwa kufanya hivyo miaka ya karibuni.
Madereva waliotoka sana nje ili kushiriki ARC ni Kirit Pandya, Pano Calavria, Ahmed Huwel, Saleh Balhabou, Navraj Hans. Issa Mohamed na Omar Bakhresa ambaye ni Mtanzania wa wa pekee aliyecheza raundi ya ARC nchini Afrika Kusini akiwa pia ameshiriki raundi za ARC nchini Tanzania, Kenya na Uganda.