Mbeya City yanogewa na ushindi

BAADA ya ushindi mnono ilioupata Mbeya City wa mabao 4-0 juzi dhidi ya Polisi Tanzania, kocha msaidizi wa kikosi hicho, Juma Bukoli amesema kwa sasa nguvu zao kubwa wanazielekeza katika mchezo ujao na Geita Gold utakaopigwa Desemba 22.

Timu hiyo iliyoshuka daraja misimu miwili nyuma, itaendelea kusalia kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kucheza dhidi ya Geita Gold, ikiwa ni vita ya kuwania nafasi mbili za juu kwa ajili ya kusaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

“Mechi itakuwa ya mbinu kali, sisi tunahitaji kukaa nafasi mbili za juu na kumaliza kwa morali mzunguko huu wa kwanza, Geita ni timu nzuri na yenye wachezaji bora ingawa tunahitaji kuutumia mchezo huo kutimiza malengo tuliyojiwekea pia.”

Nyota wa kikosi hicho, Kilaza Mazoea aliyefunga mabao matatu ‘Hat-Trick’ katika mechi na Polisi Tanzania, alisema kila mchezo kwa sasa wataucheza kama fainali ili kufikia malengo yao, licha ya kukiri ugumu wa wapinzani wanaokutana nao.

“Wachezaji kwa sasa tuna morali, ushindi wa leo (juzi) umeongeza nguvu kikosini kujiandaa na Geita Gold, safari bado ni ndefu, lakini kwa umoja na ushirikiano uliopo baina yetu tutatimiza adhima ya kucheza Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.”

Related Posts