Umuhimu upinzani, wadau kuunganisha nguvu mageuzi mfumo wa siasa

Dar es Salaam. Nguvu na sauti ya pamoja baina ya vyama vya upinzani, imetajwa kuwa hatua muhimu itakayofanikisha mageuzi ya mfumo wa siasa na Katiba ya nchi.

Kwa mujibu wa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, mkwamo wa mabadiliko ya Katiba na mfumo wa siasa nchini, unahitaji ushirikiano baina yao kushinikiza mageuzi.

Wamesema hakuna umuhimu wa kususia chaguzi, bali wanapaswa kuwa na sauti na nguvu moja itakayowalazimu watawala kubadili mifumo ya uchaguzi.

Hata hivyo, mtazamo wa ushirikiano baina ya upinzani haitakuwa hatua mpya, kwani ilishuhudiwa katika Uchaguzi Mkuu 2015.

Katika uchaguzi huo, vyama vya Chadema, ACT-Wazalendo, CUF na NCCR-Mageuzi viliungana kuunda Ukawa, kuikabili CCM katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu.

Ingawa matarajio ya kuishinda CCM katika nafasi ya urais hayakufanikiwa, angalau muungano huo uliupa upinzani viti vingi vya ubunge na udiwani zaidi ya nyakati zote za uchaguzi.

Hoja za ushirikiano wa upinzani zimetolewa jana Jumamosi, Desemba 14, 2024 na viongozi wa vyama hivyo na wadau wa siasa walipokuwa katika kipindi cha Medani za Siasa kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Star TV.

Kipindi hicho kinachoendeshwa kwa njia ya mdahalo kililenga kujadili mada ya hali ya siasa Tanzania, huku Benson Kigaila (Naibu Katibu Mkuu wa Chadema -Bara) akiiwakilisha Chadema, upande wa ACT-Wazalendo uliwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Ado Shaibu.

Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi alishiriki. Naibu Meya wa Kinondoni (CCM), Michael Urio na mwanasiasa James Mbatia hawakuhudhuria.

Licha ya tofauti za sera kwa vyama vya upinzani, Ado amesema kunahitajika ushirikiano kwenye baadhi ya mambo hasa yanayohitaji sauti moja.

Amesema kukosana wenyewe kwa wenyewe si jambo linalomnufaisha yeyote miongoni mwao, zaidi ya CCM.

Katika kufanikisha ushirikiano kwenye ajenda za mageuzi ya mfumo wa siasa na Katiba, amesema wameshaviandikia vyama ombi la kushirikiana navyo.

“Tumeviandikia barua vyama vitano, ikiwemo Chadema kuomba kushirikiana navyo katika masuala haya ya mageuzi ya siasa zetu,” amesema.

Amesisitiza umuhimu wa kupunguza minyukano baina yao, hasa ile inayowatenganisha hata kwenye mambo yanayohitaji kushirikiana.

Kigaila amesema wameshaviona vyama vyenye mawazo sawa na Chadema, hivyo wataviandikia kusudio la kushirikiana.

Ushirikiano huo kwa mujibu wa Kigaila hautahusisha kila mmoja, bali ni wale walio tayari kushirikiana kushinikiza mageuzi ya mifumo ya sheria, Katiba na siasa.

“Tunatakiwa kuunganisha nguvu za wadau wote ili kukabiliana na hawa watawala wasiotaka kubadilika wapende wasipende,” amesema.

Hata hivyo, amesema kukosekana umoja wa vyama vya upinzani wakati mwingine kunaweza kusababishwa na nguvu ya watawala.

“Tunatakiwa kuwa na umoja na ni wajibu wetu kuwa na umoja, hatutakuwa na umoja na kila mtu bali na wale ambao fikra zetu zinafanana,” amesema.

Mwabukusi amesema ushirikiano wa vyama hivyo ni jambo muhimu, lakini kunahitajika kutanuliwa wigo wa wanaoshirikiana.

Amesema si vyama vya upinzani pekee vinavyopaswa kushirikiana, bali kuwepo na wadau wengine wenye kiu na mageuzi hayo.

Amesema mchakato wa ushirikiano unapaswa ubadilishwe kutoka kuwa wa kisiasa na kuwa wa umma ili wananchi nao washiriki.

“Ninachoshawishi ni vyama kukaa pamoja na wadau kuainisha ajenda za mageuzi na kuyaendea mageuzi yenyewe,” amesema.

Amesema anakusudia kwenda mahakamani kuhoji umuhimu wa kuwepo vyama 14 vya upinzani ambavyo ataomba vifutwe.

Amedai hakuna haja ya kuhangaika na uchaguzi mkuu mwakani, badala yake itumike angalau miaka miwili kuandaa ajenda.

“Tusikimbie kwenye uchaguzi, hizi chaguzi zetu kila siku watu wanalia, hapana tufanye mageuzi kwanza,” amesema.

Alipoulizwa anaionaje hali ya siasa nchini, Ado amesema kwa sasa kuna mwelekeo mbaya zaidi akirejea uchaguzi wa serikali za mitaa.

Kwa upande wake, Kigaila amesema tatizo kubwa ni mifumo ya sheria iliyorithiwa kutoka kwa mfumo wa siasa za chama kimoja.

Amesema hakuna chama kinachotaka kupendelewa, isipokuwa wanahitaji mazingira sawa ya kucheza mchezo wa siasa.

Amesema awali Chadema waliingia kwenye mazungumzo na CCM kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan alionyesha nia njema, lakini sasa analaumiwa kwa matendo yake.

Kwa mtazamo wa Mwabukusi, nchi iliingia kwenye siasa za vyama vingi, huku ikiwa na mfumo wa chama kimoja.

“Ukiangalia majeshi yetu kwa kauli zao na viongozi wetu, wanaamini CCM ndiye mwenye haki ya kushika dola, wengine wakorofi,” amesema.

Amesema vyama vinavyoshindwa vinashindwa kujikusanya kujipanga ili vije kufanya uchaguzi, badala yake vinasumbuliwa.

Mambo hayo, ameeleza yanafanya hali isitulie, jambo linalokwaza hata chama tawala kishindwe kuongoza vema.

Amesema kumekosekana maadili yanayosababisha watu kukosea lakini hawakosolewi kwa lugha zinazostahili.

Mwabukusi amezihusisha kasoro zote hizo na changamoto iliyopo kwenye Katiba ya nchi, akisisitiza inajitaji mabadiliko.

Upatikanaji wa Katiba kwa mujibu wa Ado, unahitaji kuwa ajenda ya kila mwanamageuzi.

“Lazima twende kwenye vuguvugu kubwa la mageuzi kuwasukuma watawala waelewe kwamba tumekasirika na walazimike kuleta mageuzi,” amesema.

Kigaila amesema suala la mabadiliko ya Katiba halijafika hatua ambayo watawala wamekubali mchakato uanze.

Amesema kumekosekana utashi wa kisiasa unaofanya watawala washindwe kuridhia moja kwa moja mabadiliko ya katiba, wakihofu kukoma kubaki madarakani.

Hata hivyo, amesema ugumu wa mabadiliko ya katiba unatokana na wananchi wenyewe kushindwa kujenga nguvu ya kulazimisha hilo lifanyike.

“Tuunganishe nguvu tutengeneze uwanja sawa wa kuchezea hizi siasa. Uwanja sawa ni kuwa na sheria na katiba imara,” amesema.

Kuhusu hoja ya Katiba, Mwabukusi amesema mkwamo wa kupatikana kwake umetokana na mchakato kuhodhiwa na vyama vya siasa.

Amesema hata waliokuwa wanazungumza walifanya hivyo na walionekana kama wanataka mabadiliko ili wakashinde uchaguzi.

Amesema kiuhalisia Katiba inapaswa kuwahusu wananchi wote na iwalinde na haki zao, wakielewa kuwa Katiba ndiyo kila kitu kwao, wataona umuhimu wa kushiriki kuidai.

Related Posts