Kocha Azam awatia hasira kina Fei

KIPIGO cha mabao 2-1 ilichopewa Azam FC kutoka kwa Nyuki wa Tabora United, kimemchefua kocha wa timu hiyo, Rachid Taoussi, akisema kimewatibulia malengo, lakini akiwatia hasira wachezaji kwa kuwataka wasahau yaliyopita na kujiweka vyema kwa mchezo utakaopigwa kesho Jumanne dhidi ya Fountain Gate.

Kocha huyo raia wa Morocco, alisema matokeo waliyopata mjini Tabora yameiathiri timu na hata wachezaji kwa kiasi kikubwa, ila anajua katika soka, makosa hutokea, hivyo ni muhimu kujifunza na kuendelea mbele na mapambano.

“Kipigo ni sehemu ya mchezo, tulifanya makosa na yakatuumiza, ila kwa sasa tunapaswa kukubali na kujirekebisha, hasa kwa mechi ijayo ambayo kwetu ina umuhimu mkubwa zaidi katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara,” alisema Taoussi

Alissema licha ya makosa yaliyojitokeza hasa kwa kipa Mohamed Mustafa, ni muhimu kujua kila mchezaji ana jukumu lake uwanjani na mchezo mmoja hauwezi kubadili kila kitu.

Taoussi aliwakumbusha wachezaji, ingawa kipigo hicho kilikomesha mfululizo wa ushindi wa mechi saba, bado Azam ipo kileleni mwa msimamo na pointi 30, hivyo ni lazima wachezaji wote kupambana ili kuendelea kuifanya timu hiyo iwe bora zaidi na kufikia malengo waliyojiwekea.

“Niliwaambia, wasijali kuhusu matokeo hayo. Hatuwezi kubadili kilichopita, lakini tunaweza kuamua kile kitakachofuata. Mchezo dhidi ya Fountain Gate ni muhimu katika safari yetu,” aliongeza kocha Taoussi.

Mchezo ujao, Taoussi anajua utakuwa na changamoto kubwa, kwani Fountain Gate inayoshika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi, ina uwezo mkubwa wa kushambulia na katika mchezo uliopita iliifunga Coastal Union kwa mabao 3-2, pia ikiwa ni timu iliyofunga mabao mengi, licha ya kuwa na ukuta mwepesi vilevile ikifunga 23 na kufungwa idadi kama hiyo.

“Ni timu ya hatari, lakini sisi pia tunayo silaha yetu. Lazima tushambulie kwa umakini na kuimarisha ulinzi wetu,” alisema Taoussi.

Kocha huyo alifafanua, katika soka hakuna timu isiyokosea na hiyo ndiyo maana ni muhimu kwa wachezaji wake kuwa na uvumilivu na kupambana hadi mwishoni. Alikiri, kipa Mohamed Mustafa alifanya makosa ya kiufundi katika mchezo dhidi ya Tabora United, lakini alisema ni sehemu ya mchezo na anatarajia atarudi mwenye nguvu zaidi.

Related Posts