Dar Kings imeendelea kufunika katika Ligi ya TCA kwa vijana wa umri chini ya miaka 17, kwenye viwanja vya UDSM na Dar Gymkhana, baada ya kuifumua Gairo Kings kwa mikimbio 22.
Ligi hiyo ya mizunguko 30 inajumuisha timu za vijana kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania na licha ya ushindi huo, , Dar Kings ilipata upinzani mkali kutoka kwa Gairo, waliodhihirisha ubora wao.
Dar Kings ndiyo iliyoanza kubeti ikifikisha mikimbio 244 na hadi mwisho wa mzunguko wa 30, ilipoteza wiketi sita, huku Gairo ikipambana kuifikia, kabla ya kugota katika mikimbio 222 , kwa mizunguko yote 30, ikipoteza kwa mikimbio 22.
Ushindi wa Dar Kings ulibebwa na Johnson David aliyepiga mikimbio 127 bila ya kutoka kupitia mipira 89, huku Salman Yasser akitengeneza 23 na Dev Mandania 22.
Katika mchezo mwingine, Tanga Kings iliondoka na ushindi mnono wa mikimbio 83 dhidi ya United Kings.
Tanga ndiyo iliyoanza kubeti na kutengeneza mikimbio 132 baada ya kumaliza mizunguko yote 30, ikipoteza wiketi 9.
Ilikuwa kazi pevu kwa United Kings kupata mikimbio 132, kwani walichopata ni mikimbio 49 tu baada ya wote kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 13 kati ya 30.
Nyota wa mikimbio katika mechi hiyo ni Feisal Mohamed aliyepiga mikimbio 31 akisaidiwa na Wingu Mohamed, mikimbio 13
Combined Kings waliifunga Arusha Kings kwa mikimbio 63 na ndio waliokuwa wa kwanzakupata kura ya kuanza kubeti, huku wakitengeneza mikimbio 144 baada ya kumaliza mizunguko yote 30 na kupoteza wiketi tano na wapinzani wao wakiishia mikimbio 81 baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 23 kati ya 30, hivyo kupoteza mechi kwa mikimbio 63.
Baraka Fredy ndiye aliyeibeba Combined United kwa kutengeneza mikimbio 37 akisaidiwa na Mustafa Shaban aliyepiga mikimbio 30.