MSHAMBULIAJI wa Fountain Gate, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ huenda akauwahi mchezo wa keshokutwa Jumanne kati ya timu hiyo na Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi Dar es Salaam, baada ya kukosekana michezo miwili mfululizo iliyopita kutokana na kusumbuliwa na majeraha.
Nyota huyo mwenye mabao sita ya Ligi Kuu ameng’olewa kilele cha wafungaji na Mkenya Elvis Rupia wa Singida Black Stars aliyefunga saba, amekosekana michezo miwili baada ya kusumbuliwa na majeraha ya nyama za paja, ingawa kwa sasa anaendelea vizuri.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwalimu alisema yupo fiti, tayari kucheza baada ya kukosekana mechi zilizopita, huku akiweka wazi shauku yake kubwa ni kuona akiendelea tena kufunga kutokana na kuandamwa na ukame wa mabao.
“Kwa sasa naendelea vizuri na kama benchi la ufundi likiwapendeza naweza nikacheza mechi ijayo dhidi ya Azam, ni kweli kwa siku za karibuni nimeshindwa kuonekana, ila niwaambie mashabiki zangu waendelee kusubiria kwani mambo mazuri yanakuja,” alisema Mwalimu aliyesajiliwa msimu huu akitokea Zanzibar.
Kwa upande wa kocha Mohamed Muya alisema baada ya nyota huyo kupata majeraha hayo hakutaka kuhatarisha afya yake, ingawa kuna muda alikuwa anahitaji acheze aisaidie timu kutokana na matokeo mabaya waliyokuwa wanayapata.
“Baada ya matokeo mabaya kabla ya mchezo wetu wa mwisho na Coastal Union alikuwa anatamani sana acheze lakini niliamua kumpa muda wa kujiuguza ili apone vizuri, kwa sasa yupo fiti na kuna uwezekano mkubwa akacheza michezo yetu inayofuata.”
Mshambuliaji huyo alikosa mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya 64, dhidi ya Mweta Sports ya Mwanza ambao Fountain Gate ilishinda mabao 2-0, kisha akakosa uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union walioshinda 3-2.
Mara ya mwisho kwa nyota huyo kufunga katika Ligi Kuu Bara ilikuwa ni ushindi wa kikosi hicho wa mabao 3-1 dhidi ya KMC siku ya Oktoba 21 na kuanzia hapo hajafunga tena hadi leo, akikaribia miezi miwili bila ya kuona nyavu za wapinzani.