CS Sfaxien yarusha ngumi Kwa Mkapa

BAO  la dakika za lala salama lililofungwa na Kibu Denis limegeuka chanzo cha vurugu kubwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, baada ya Simba SC kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia kwenye mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mwamuzi wa mchezo, Andofetra Avombitana kutoka Madagascar, alikumbana na presha  kubwa mara baada ya filimbi ya mwisho kutoka kwa wachezaji wa CS Sfaxien, ambao walimzonga wakidai kutoridhishwa na maamuzi yake ya mchezo huo.

Vurugu hizo zilichukua zaidi ya dakika 10, zikihusisha wachezaji na baadhi ya maofisa wa Sfaxien ambao walionekana kuchochea hali hiyo.

Hatimaye, walinzi wa usalama wa uwanjani (stewards) walilazimika kuingilia kati, wakimsindikiza mwamuzi nje ya uwanja chini ya ulinzi mkali. 

Baadhi ya nyota wa CS Sfaxien hawakuishia kwa kumzonga mwamuzi pekee, bali pia walirushiana maneno na stewards, hali iliyowafanya kushikana mashati.

Hali ilipozidi kuwa mbaya, askari wa Jeshi la Polisi waliingia uwanjani kuhakikisha usalama. 

Aidha, vurugu hizo zilichochewa zaidi na mashabiki wachache wa Simba waliovuka uzio na kuingia uwanjani, wakiongeza mvutano na hali ya taharuki.

Polisi walifanikiwa kuwatuliza wahusika, na baada ya muda mambo yalirejea kuwa shwari. 

CS SFAXIEN WAGOMA UWANJANI

Baada ya vurugu hizo kupungua, wachezaji wa CS Sfaxien waligoma kurejea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwa zaidi ya dakika 30.

Badala yake, walikaa makundi kwenye benchi lao la ufundi huku wakionekana kushikilia msimamo wa kutafuta suluhu ya malalamiko yao. 

Stewards walilazimika kutengeneza mduara na kuwaweka wachezaji wa Sfaxien katikati kwa ajili ya usalama wao, wakisubiri amri kutoka kwa viongozi wa mchezo. 

Licha ya vurugu hizo, mashabiki wa Simba waliondoka uwanjani wakiwa na furaha kubwa baada ya ushindi huo muhimu, ambao unaimarisha nafasi yao kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo ya kimataifa.

Bao la kwanza la Simba lilifungwa na Kibu katika dakika ya saba ikiwa ni la kusawazisha, baada ya kutanguliwa mapema na Sfaxien. Denis tena alifanya yake kwa kuihakikishia Simba ushindi kwa bao la  dakika za majeruhi. 

Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa kuhusu nidhamu ya wachezaji na maofisa wa timu ya CS Sfaxien, huku hatua zaidi za kinidhamu kutoka kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) zikisubiriwa.

Related Posts