Dar es Salaam. Kutolewa kwa pensheni za kila mwezi, afya bure kuanzia ngazi ya msingi, ajira, mikopo na elimu jumuishi ni miongoni mwa vitu vilivyotawala katika ukusanyaji wa maoni rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kundi la watu wenye ulemavu.
Kutolewa pensheni, kunatajwa kuwa moja ya njia ya kupunguza makali ya maisha kwa watu hawa ambao mara nyingi huhitaji usaidizi wa watu wengi.
Maoni hayo yametolewa na kundi la watu wenye ulemavu katika mkutano wa pili ulioandaliwa na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kupitia Tume ya Mipango na Uwekezaji ukilenga kukusanya maoni ya rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyozinduliwa Desemba 11, 2024.
Ukusanyaji maoni ya rasimu hiyo utakamilishwa Januari 12, 2025 ili kutoa wigo kwa wataalamu kukamilisha rasimu ya pili ya dira ambayo itapokelewa Januari 18, 2025 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Akizungumza katika mkutano huu leo Jumapili, Desemba 15, 2024, Joseph Sanga kutoka Taasisi ya utetezi wa haki na mahitaji ya watu walioathirika kisaikolojia (Tuspo), ameitaka Serikali itoe pensheni kwa watu wenye ulemavu ili kuweka urahisi kwao kumudu baadhi ya mahitaji.
“Tupate pensheni kwa ajili ya kujikimu, ikiwemo kupata chakula kwa sababu tunakunywa dawa ambazo zinahitaji upate chakula cha kutosha,” amesema Sanga.
Kuhusu mikopo, amesema wamekuwa wakibaguliwa kwa kuonekana hawana akili timamu, jambo ambalo pia huenda sambamba na kukosa fursa za ajira.
“Dawa pia tupewe bure, watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) wanapewa bure na sisi tupewe bure,” amesema.
Suala la utoaji pensheni liliungwa mkono na Lupi Mwaisaka kutoka Chama cha Viziwi Tanzania, aliyesema nchi nyingine watu wenye ulemavu wanalipwa pensheni kila mwezi kulingana na uzito wa ulemavu wake, ila kwa Tanzania jambo hilo hakuna.
Pamoja na kukosekana kwake, amesema hata ruzuku iliyokuwa ikitolewa awali na Serikali kwa vyama vya watu wenye ulemavu imeondolewa, jambo linalowafanya kujiendesha kwa kuchangishana fedha.
“Serikali iangalie namna ya kupunguza kodi kwa watu wenye ulemavu isiwe sawa na wasiokuwa na ulemavu, ili kutusaidia, kwani zamani tulikuwa tunapatiwa ruzuku na Serikali, lakini sasa haitolewi. Tunaomba Serikali ifikirie hili,” amesema Lupi.
Kutoka kikundi cha sanaa na utamaduni cha viziwi Tanzania, Habibu Mrope ameitaka Serikali kufanya utafiti kwa kuangalia kimataifa mengine namna wanavyowapa pensheni wenye ulemavu kulingana na hali ya nchi.
“Hii itasaidia wenye ulemavu kuishi maisha yetu vizuri. Pia tunaomba Serikali ikutane na sisi kila wakati tujadiliane namna ya kutatua changamoto zetu na tutoe shuhuda namna changamoto zetu zimetatuliwa,” amesema.
Mbali na pensheni, David Shaba amependekeza kuwapo bajeti maalumu inayoshughulikia watu wenye ulemavu ambayo itasimamiwa na wizara ndogo ya watu wenye ulemavu.
Mwenyekiti wa wanawake na watoto wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulamevu Tanzania (Shivyawata), Nuru Awadhi ametaka dira iseme wazi kuwa lugha ya alama ni lazima itolewe kwa wanaosoma elimu ya afya, ili kuweka urahisi wa utoaji huduma kwa wenye ulemavu wanapokwenda hospitalini.
“Hospitali zote tunapokwenda kulazwa pia turuhusiwe kuwa na mtu ninayemuamini kwa sababu tuna ushuhuda wa mtu wetu ambaye haoni alijifungua pacha, lakini aliibiwa mtoto mmoja, lakini kama angekuwepo mtu mwingine ingemsaidia,” amesema.
Katibu Mkuu wa Shivyawata, Jonas Lubago ametaka huduma za afya hasa afya ya akili, matibabu ya macho, huduma za utengamao, ngozi kwa wenye ualbino zishuke kuanzia ngazi ya msingi, ili watu hao wasifuate huduma mbali, jambo linalowakosesha huduma na kuwafanya kubaki katika shida hiyo.
“Pia tuweke nguvu katika kukinga na kuzuia ulemavu, mkakati uwekwe, kwani Shirika la Afya Duniani (WHO) wanasema asilimia 80 ya ulemavu unazuilika kupitia chanjo,” amesema Lubago.
Pia alitaka dira kuweka kipaumbele kulinda usalama wa watu wenye ualbino ili kuhakikisha vitendo vya ukatili, unyanyasaji vinaondoshwa.
Chama cha Wasioona Tanzania, kimetaka Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iwakikishie watu wenye ulemavu matibabu bure kwa asilimia 100.
Akitoa maoni, Francis Daula amesema baadhi ya hospitali wanaonana na madaktari bure, lakini inapofika suala la dawa imekuwa changamoto na hasa inapohitajika matibabu zaidi kama upasuaji.
Katika upande wa miundombinu ya kujifunzia, Rehema Ibrahim ametaka vyuo vikubwa vya Serikali viwe na namna ya kuweka miundombinu wezeshi hasa katika upande wa teknlojia kwa ajili ya wenye ulemavu kama ilivyo kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ili kuweka ujumuishi katika elimu.
Stella Jailos, ametaka kuwapo kwa mpango mkakati ili kuwezesha kuongeza ushiriki wa wenye ulemavu katika ngazi mbalimbali za maamuzi.
Akifunga mjadala huo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga amewataka waandishi wa dira kuzingatia maoni yaliyotolewa na watu wenye ulemavu.
“Niwahakikishie wenzangu wenye ulemavu kuwa maoni yenu yote yatafanyiwa kazi,” amesema Nderiananga.
Akizungumzia ruzuku kwa wenye ulemavu, amesema mwaka 2018 alipelekwa Japan na Thailand kuona mamna nchi hizo zinavyowezesha watu wao wenye ulemavu, huku akiweka wazi kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anachukulia kwa uzito suala la wenye ulemavu.