Mwanza. Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martin Nkwabi ametaja changamoto tano zilizoko kwenye magari ya shule yanayowafuata na kuwarudisha wanafunzi nyumbani, huku akipiga marufuku magari hayo kuwa na vioo visivyoonyesha aliyekaa ndani ‘tinted’.
Amesema changamoto nyingine ni madereva kukiuka muda wa kuwafuata na kuwarudisha wanafunzi nyumbani na ukosefu wa wahudumu wa kike, wamiliki wa shule kununua magari chakavu na wafanyakazi kukosa uadilifu, jambo linalohatarisha usalama wa wanafunzi.
Nkwabi amesema hayo leo Jumapili, Desemba 15, 2024 alipozungumza na wamiliki wa shule, wasimamizi wa sheria, madereva na wadau wa usafirishaji mkoani humo.
Amesema amepiga marufuku magari yenye tinted kutumika kubeba wanafunzi kwa kuwa yanatishia usalama wa wanafunzi.
Pia amesema kutokana na umbali wa sehemu za wanafunzi wanakoishi, madereva wengi huwachukua kuanzia saa 10 usiku, huku baadhi wakiwarudisha nyumbani saa tatu mpaka nne usiku kinyume cha sheria.
“Wakati wa kurudi wanafunzi wanarudishwa mpaka saa tatu au nne usiku, unajiuliza huyu mwanafunzi anapumzika saa ngapi kama huyo huyo saa 9 anaamshwa kwa ajili ya kujiandaa, gari la wanafunzi haliruhusiwi kutembea likiwa limebeba wanafunzi zaidi ya saa 11 jioni,” amesema.
Akizungumzia wahudumu wa wanafunzi amesema miongozo inaelekeza kila gari la shule linatakiwa kuwa na mhudumu jinsia ya kike ama wahudumu wa kike wawili ama mmoja kati ya wahudumu wawili awe mwanamke.
Ofisa Mfawidhi Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Maria Chacha, mbali na changamoto hizo, amewaomba madereva kujisajili na kufanya mtihani wa LATRA ili kutambulika katika mamlaka hiyo.
“Usikubali kuendesha chombo cha wanafunzi huku kikiwa hakina leseni, pia hakikisha hilo gari limepakwa rangi ya njano na yawe yamekaguliwa na Polisi. Nawasisitiza madereva jisajilini, mthibitishwe kwa kufanya mtihani wa Latra ili kuhakikisha kama kweli una mafunzo ambayo yanakufanya kuwa na sifa ya kubeba hao watoto,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Aloyce Nyantora kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amewataka wamiliki na madereva wa magari ya shule kuyapeleka magari yao yakakaguliwe na kupewa hati ya utambulisho.
“Tutumie kipindi hiki cha likizo, kabla shule hazijafunguliwa kukagua magari yenu, muda wa kufungua shule ukikaribia tutakuwa wakali na magari yote ambayo yatabainika kuwa mabovu au hayajafanyiwa marekebisho hatua kali za kisheria zitachukuliwa,” amesema.
Nyantora amesema oparesheni ya Juni 2024 yalikaguliwa magari 252 na kwamba kati ya hayo 217 yalikuwa na hali nzuri, huku magari 35 yalikuwa mabovu na kutakiwa kufanyiwa ukarabati.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Mwanza, Mrakibu wa Polisi, Sunday Ibrahim amesema kazi ya ukaguzi wa magari ya shule imeanza jana na itahitimishwa mwishoni mwa Desemba 2024, huku ikiambatana na utoaji elimu na kukabidhi hati ya kutambua endapo gari limekaguliwa.