Mwanza. Maeneo ya fukwe za Ziwa Victoria yameendelea kuwa hatarishi kwa wakazi wake kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya wanyama wakali kama mamba na viboko hali inayosababisha vifo na majeraha kwa watu.
Hili linawaibua wadau kama polisi na wataalamu wa afya kutoa mwongozo wananchi wanapopatwa na madhila haya.
Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake jijini Mwanza, kuhusu umuhimu wa fomu ya matibabu (PF3), ofisini kwake Kamanda wa Polisi jijini humo, Wilbroad Mutafungwa anasema kuwa ni kweli kuna changamoto kwenye maeneo ya fukwe za Ziwa Victoria ya watu kushambuliwa na mamba na kwa uchache kupoteza maisha.
Anasema Jeshi la Polisi likiripotiwa kuwapo kwa madhara huwa wanakwenda kukagua ambapo lazima waende na fomu ya matibabu (PF3) kwa majeruhi ambapo itakuwa imejazwa taarifa za mgonjwa, ambazo zitamsaidia masuala mengine ya kisheria.
“Tukio lisiporipotiwa siyo rahisi sisi kutoa hati ya matibabu (PF3), wanawatibia vipi bila hiyo fomu ni suala la watoa huduma ya afya, ila sisi huwa tunatoa elimu kuhusu suala hilo kila mara hasa kwenye maeneo ya fukwe” anasema Mutafungwa.
Akizungumzia sababu za watu walioliwa na mamba kupata ganzi kwenye majeraha Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kome , kilichopo kijiji cha Buhama, Dk Juma Shagambe Juma anasema hali hiyo inatokana na meno ya mamba kukata mishipa midogomidogo ya fahamu na inayopitisha damu, hivyo damu haiendi ipasavyo.
“Kwa sababu ni matatizo ya muda mrefu muathirika anaweza kupona kwa kufanya mazoezi atakayoshauriwa na daktari lakini hatapona mara moja, atachukua muda,”anasema Dk Juma.
Anasema madhara ya papo kwa hapo ni kupoteza damu nyingi, huku kuhusu sumu akisema kuwa mamba anapomng’ata mtu hatoi sumu moja kwa moja na ndiyo maana walio wengi wakipata tiba wanapona.
Watoto wanaathirika zaidi
Ilikuwa siku ya Ijumaa kama zilivyo nyingine tuliamka na mke wangu tukaenda shamba, tukarudi mchana tukala kama familia, kisha tukaenda tena shambani watoto wakaenda ziwani ambako huchota maji, kufua na kuosha vyombo.
Tukiwa shambani aikuja binti anakimbia na kutueleza Mata ameliwa na mamba, tulistuka na baada ya hapo mimi na mke wangu kilan mmoja alikimbia na njia yake tukakutana ziwani haa karibu na nyumbani, kweli tukakuta Mata amechukuliwa na mamba na hayupo kabisa eneo hilo.
“Tukamtafuta mpaka usiku bila mafanikio, kesho yake muda wa saa nane akaibuka akiwa ameshaliwa mguu na utumbo tukachukua mwili tukarudi nao nyumbani kwa ajili ya mazishi,”anasema Maiko Michael baba wa watoto wanane na mkazi wa Kijiji cha Nyachitale, Kata ya Buhama, Halmashauri ya Buchosa.
Anasema hayo ni maeneo ambayo wanakwenda watu siku zote alikuwa na miaka 12 akisma darasa la tano Shue ya Msingi Buhama.
“Mamba ni wengi lakini wanajifichaficha, kuna wakati wanaonekana kila siku lakini kuna kipindi wanapotea wiki nzima, tukiona kuna mamba tunajihadhari. “Nimezaliwa hapa kwa sasa nina miaka 41, matukio ya watu kuliwa na mamba nimeshuhudia kama mara nne hivi, Buhama alikamatwa mmoja, Nyachitale alikamatwa mwingine, mwingine alijeruhiwa mguu ikamuacha na mwingine hapahapa nimeshayashuhudia watu wakiliwa na mnyama huyo.
Akilizunumzia hilo mama mzazi wa marehemu Mata, Joyce Chengesa anasema Serikali imejenga vizimba kwa ajili ya kukoga na kufanya shughuli nyingine lakini havitoshi.
Joyce anasema kwa wakazi wa ziwani kuwatenganisha na ziwa si rahisi sana, hivyo Serikali ije na utaratibu wa kukabiliana na huu wingi wa mamba.
“Mata wangu ameniuma sana alikuwa ameshakuwa binti wa kumtegemea lakini mamba amekatisha maisha yake, ni mnyama nisiyemsamehe hata nikimuona anaona hasira sana, Serikali iangalie namna ya kufanya watoto wetu wapo mashakani na kwa ujumla maisha ya visiwani kwa sasa ni hatari tupu tunawindwa na wanyama tusioweza uwadhibiti kwa namna yoyote ile,”anasema Joyce.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Chubize Enus anasema kuwa mwaka 2023 wakiwa kwenye msiba wa shemeji yake walipomaliza kua chakula cha mchana vijana na watoto wakaenda kukoga ziwani.
Anasema wakiwa huko walipomaliza kukoga wakatoka ziwani salama na kuanza kuondoka, lakini mtoto wake (marehemu John Evod aliyekuwa na miaka tisa akisoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Buhama) akaanza kurudi ziwani, wenzake wakaamuuliza unakwenda kufanya nini jua limeshazama huko kuna mamba?”
Hata siji mtoto wangu alikutwa na nini, akawajibu wenzake kuwa anakwenda kunawa anaona miguuni ana michanga huku akiwaonyesha ilihali ukimaliza kukoga ziwani michanga ni kitu cha kawaida, wakamzuia wakashindwa akarudi ziwani hakuchukua muda akachukuliwa na mamba.
“Tulimtafuta kwa siku mbili bila mafanikio tukaupata mwili siku ya Jumapili katika kijiji kingine cha Nfunzi utumbo ukiwa umeliwa, amejeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili,”anasema Chubize mama mzazi wa marehemu.
Richard Enus, baba mdogo wa marehemu Evod anasema kuwa pamoja na madhara hayo Serikali mpaka sasa haijawapa hata mkono wa pole.
“Kwanza masharti ni mengi mno hadi angalau uwekewe kwenye orodha ya watakaopatiwa hayo malipo wanayosema ni mkono wa pole, lakini huwezi kujua nini kinaendelea huko kwani miaka inakatika na hakuna aliyewahi kulipwa licha ya kuandikishwa huku na kule.”
Anasema licha ya kutumia gharama nyingi kwenda na kurudi Halmashauri ya Buchosa kuonana na watu wa wanyamapori kwa ajili ya kupewa mkono wa pole, hakuna alichoambulia na sasa ameamua kumuachia Mungu.
Tawa kuvuna mamba kupunguza madhara
Akizungumzia hatua wanazochukua kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu wakiwamo mamba, Mohammed Omar Mpita, Ofisa Uhifadhi daraja la Kwanza kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) Kituo cha Mwanza, anasema wanafanya kazi katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita na Kagera.
Anasema wanapata matukio ya wanyama wakali mkoani Mwanza wakiwamo fisi, mamba na kiboko, ambapo changamoto zaidi wanaipata katika wilaya ya Sengerema yenye halmashauri mbili ya Sengerema na Buchosa.
“Kutokana na kupata matukio hayo ya kudhuru watu Sengerema tumelifanya eneo la kimkakati kwa kuweka vikosi viwili vinavyopishana kwenda kufanya kazi eneo hilo ambapo hubadilishana kila baada ya siku 15, lengo ni kuhakikisha linapotokea tukio kuhusu wanyama hao askari wawe jirani kutoa msaada.”
Anasema Julai 2024 mpaka Novemba wameua mamba 20 na viboko wawili.
Anasema kutokana na mamba kuwa na matukio mengi ya kudhuru binadamu hivi karibuni Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa ruhusa ya kuvuna mamba.
“Lengo ni kujaribu kupunguza madhara, maana matukio kwenye Ziwa Victoria ni mengi, mengine yanatufikia, mengine hayatufikii. Kwa kuanzia tutavuna mamba 17, ambapo watu wa Tawa wapo huko wanaagalia wanawavunaje.
Anasema katika kuhakikisha wanatoa msaada kila unapohitajika wanapokea taarifa kutoka kwa viongozi wa halmashauri ya wilaya na watendaji wa vijiji pindi wanyama wanapoonekana na kuleta madhara kwa wananchi.
Takwimu
Anasema kuanzia mwaka 2023 mpaka Julai 2024 mamba wamesababisha vifo 13, fisi wamesababisha viwili huku fisi wakisababisha pia majeruhi watano na wawili samebabishwa na mamba.
“Inawezekana kuna taarifa zipo kwa wananchi huku ofisini hazijatufikia, kwani haya matukio ni mengi,”anasema Kamanda Mpita.
Itaendelea kesho kuona mabadiliko ya tabianchi yanavyohatarisha wanyama kutoweka.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917