Dar es Salaam. Kukua kwa mahitaji ikilinganishwa na uwepo wa bidhaa husika sokoni, kumetajwa kuwa sababu ya ongezeko la bei katika kipindi cha Desemba kila mwaka.
Hali hiyo huchangiwa na idadi ya watu wanaokuwapo nyumbani wakati wote wa Desemba, utamaduni wa watu kununua bidhaa nyingi, ikiwemo nguo na kufanya manunuzi mbalimbali kunatajwa kusisimua biashara.
Haya yanaelezwa wakati ambao Mwananchi imefanya uchunguzi na kubaini kuwapo ongezeko la bei katika baadhi ya bidhaa za vyakula katika masoko mbalimbali jijini Dar es Salaam, ikiwemo mchele, mafuta ya kupikia, mbogamboga, vitunguu na nyama.
Wakati hali ikiwa hivyo masokoni, mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Novemba, 2024 umebaki katika asilimia 3.0 kama ilivyokuwa mwaka ulioishia Oktoba, 2024 kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Kwa upande wa mchele, Seleman Issa, ambaye ni mchuuzi anasema kumekuwa na mabadiliko ya bei ya jumla katika soko la Tandale ambako sasa mchele mzuri (super) kilo moja ni kati ya Sh2,500 hadi Sh2,600 kutoka Sh2,000 hadi Sh1,800.
Mchele wa kawaida sasa unauzwa kati ya Sh2,000 hadi Sh1,700 kutoka Sh1,500 bei ambazo zimepanda kuanzia wiki iliyopita.
“Kupanda kwa bei hakuhusiani na sikukuu, bali kipindi hiki si msimu wa mavuno ndiyo maana hali ipo hivyo na utaendelea kupanda. Sikukuu hizi wala mchele hauliwi sana ukilinganisha na ndizi na viazi,” anasema Issa.
Mafuta ya kupikia nayo yanaelezwa kupanda bei ndani ya wiki iliyopita.
Mfanyabiashara wa bidhaa za jumla na rejareja, Emmanuel Gerald, mkazi wa Chanika anasema mafuta ya kupikia lita tatu yaliyokuwa yakiuzwa Sh16,000 sasa yanauzwa Sh18,000, huku yale ya lita tano yaliyokuwa yakiuzwa Sh25,000 kwa sasa yanauzwa Sh27,000.
Ndoo ya mafuta lita 10 amesema inauzwa Sh95,000 kutoka Sh93,000, huku lita moja ikiuzwa Sh4,800 kutoka Sh4,600.
Masoud Fahamu, mfanyabiashara wa mbogamboga katika soko la Mabibo anasema kiroba cha karoti kilichokuwa kikiuzwa Sh50,000 sasa ni Sh80,000 na zimepanda wiki iliyopita.
Kilo ya karoti inauzwa kati ya Sh1,500 hadi Sh2,000 wakati awali iliuzwa kati ya Sh1,500 na Sh1,100.
“Hii imechangiwa na kutopatikana shambani na sasa wengi wanachukua nchini Kenya,” anasema.
“Karoti kawaida zikiwa nyingi sokoni hupatikana mikoa ya Arusha na Tanga, lakini kwa kuwa hizi za sasa zinavuka mpaka na hadi zitoke huko kutufikia ni gharama imetumika, ndiyo maana unaona bei yake imechangamka sokoni,” amesema Fahamu.
Kuhusu pilipili hoho, amesema hivi sasa imeshuka kutoka Sh70,000 hadi Sh50,000 kwa kiroba ukilinganisha na Novemba kurudi nyuma.
Vitunguu maji vimepanda kutoka Sh110,000 hadi Sh130,000 kwa gunia huku nyanya zikiuzwa kati ya Sh40,000 hadi Sh50,000 kutoka Sh20,000 hadi Sh15,000 iliyokuwa awali.
“Kwa nyanya sababu imechangiwa na mikoa mingi hivi sasa mvua zinanyesha, hivyo kutokuwa rahisi kuzifikisha sokoni,” amesema Fahamu.
Katika soko la Mabibo, mfanyabiashara Zahoro Mfaume amesema gunia moja la viazi limepanda kutoka Sh65,000 na sasa ni kati ya Sh80,000 na Sh85,000 huku sado iliyokuwa ikiuzwa Sh3,000 sasa ni Sh5,000.
Amesema ndizi zinazotoka Morogoro na Mbeya hazijapanda bei kwani mkungu unauzwa kati ya Sh40,000 hadi Sh50,000 wakati mshare kutoka Moshi zikiuzwa kati ya Sh70,000 kutoka Sh50,000 hadi Sh60,000 iliyokuwa awali.
Kwa upande wa viungo, vitunguu saumu kilo moja inauzwa Sh22,000 kutoka Sh10,000 iliyouzwa Novemba.
Wakati bidhaa nyingine zikiongezeka bei, tangawizi imeanza kushuka. Awali kilo moja iliuzwa Sh8,000 sasa ni Sh6,000 hadi Sh5,000.
Kwa upande wa malimao sasa ni Sh150,000 kutoka Sh190,000 hadi Sh200,000 bei iliyokuwa miezi miwili iliyopita.
Nyama bei ya wastani ya mifugo katika mnada wa Pugu kwa wiki inayoishia Desemba 13, 2024 imeshuka ukilinganisha na wiki iliyopita.
Hali hiyo inaelezwa imesababishwa na kuongezeka kwa ugavi wa mifugo mnadani.
Katika wiki hiyo, ng’ombe mwenye uzito wa kilo 300 na zaidi aliuzwa Sh3.3 milioni kutoka Sh3.4 milioni wiki iliyotanguliwa, ng’ombe mwenye uzito kwa kilo 195 alisalia Sh2.05 milioni sawa na wiki iliyotangulia.
Hata hivyo, ng’ombe mwenye uzito wa kilo 90 alifikia Sh800,000 kutoka Sh750,000 katika wiki iliyotangulia. Bei hii inaendelea kuimarika wakati ambao wananchi wanaendelea kuugulia maumivu ya kupaa kwa bei za nyama za rejareja mitaa.
Katika baadhi ya maeneo hivi sasa kilo moja imefikia kati ya Sh14,000 na Sh13,000 kutoka Sh8,000 hadi Sh9,000 iliyokuwapo miezi michache iliyopita.
Samaki imefikia Sh14,000 kwa kilo katika baadhi ya maeneo kutoka Sh11,000, huku sukari ikiendelea kubaki kati ya Sh2,800 na Sh2,600 kwa kilo.
Kubaki kwa wastani wa asilimia tatu ya mfumuko wa bei kitaifa katika mwaka ulioishia Novemba 2024 kwa mujibu wa NBS inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Novemba, 2024 imebaki sawa na kasi iliyokuwa kwa mwaka ulioishia Oktoba, 2024.
Hata hivyo, fahirisi za bei zimeongezeka kutoka 112.67 Novemba, 2023 hadi 116.05 Novemba, 2024.
Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Novemba, 2024 umeongezeka hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 2.5 kwa mwaka ulioishia Oktoba, 2024.
Kwa upande mwingine, mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Novemba, 2024 umepungua hadi asilimia 2.9 kutoka asilimia 3.2 kwa mwaka ulioishia Oktoba, 2024.
Mtaalamu wa uchumi na biashara, Dk Donath Olomi amesema kupanda kwa bei mara nyingi huangaliwa na mahitaji yaliyopo sokoni ikilinganishwa na bidhaa zilizopo sokoni.
Amesema ikikaribia sikukuu mahitaji yanakuwa makubwa, kwani ndiyo muda ambao watu hufanya manunuzi makubwa, ikiwemo kununua nguo na vyakula.
Jambo hilo ndilo huvutia bei kuongeza si sokoni pekee, bali kuanzia sehemu ambayo wanunuzi wa rejareja huchukulia.
“Msimu kama huu ndiyowafanyabiashara huutumia kupata faida, pia ni msimu ambao kuna baadhi ya biashara huuzika sana kuliko mingine yoyote, hivyo ni jambo la kawaida kushuhudia mabadiliko ya bei,” amesema Dk Olomi.
Kupanda kwa bei kuna athari za moja kwa moja kwa wananchi ambao ndio watumiaji wa mwisho wa bidhaa kutokana na kupunguza uwezo wao wa kumudu gharama za maisha.
Shani Abdul, mkazi wa Tabata amesema ongezeka la bei limetokea wakati ambao familia nyingi ziko nyumbani jambo ambalo linaongeza gharama za maisha.
“Siku za kawaida watoto wako shuleni, gharama inapungua kidogo kwa sababu bajeti unayowaza ni jioni, ila hivi sasa unaumiza kichwa kuanzia asubuhi, mchana na jioni, bei ndiyo hizi ziko juu,” amesema Shani.
Zaida Masanja, amesema bei zimesababisha kutafuta njia mbadala, ili familia zipate chakula cha kila siku.
“Watakula, lakini tutaangalia vitu vya bei rahisi, hizi nyama, samaki kwa kweli hapana, hela ni ngumu,” amesema.