Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ametaka kila mmoja ajitahidi kufanya jambo la heri kwa mwenzake badala ya kumuumiza.
Amesema kila mmoja awe baraka kwa wengine na siyo kitunguu cha kuwatoa watu machozi.
Ametoa rai hiyo leo Jumapili, Desemba 15, 2024 jijini Dar es Salaam alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kutabaruku Kanisa la Waadventista Wasabato, Magomeni.
Amewataka Watanzania kujenga misingi ya kusaidiana, kuheshimiana na kuvumiliana ili kufanikisha malengo wanayojiwekea kimaendeleo.
Dk Biteko amewahimiza waumini na Watanzania kwa ujumla kuboresha huduma za jamii na kuwekeza katika mipango itakayowezesha kukidhi mahitaji na kupata Taifa endelevu.
“Rais (Samia) siku zote amekuwa akisisitiza maridhiano, uhimilivu, mabadiliko na kuimarisha amani yetu ili jamii ipate maendeleo na kustawi,” amesema.
Amewataka waumini kuendeleza moyo wa kujitolea kwa ajili ya uwekezaji na ujenzi wa miundombinu ya maendeleo kama vile kanisa na miradi mingine ya kijamii.
Kwa mujibu wa Dk Biteko, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha misingi ya malezi na ushirikiano inayowekwa inafanikiwa.
“Wametajwa baadhi ya watu waliofanikisha ujenzi wa kanisa hili la Magomeni, lakini pia wapo ambao hawakutajwa kwa kuwa hawakuwa tayari kutajwa na hii ndiyo sababu kwao kutotajwa, sasa tuanze upya kila mmoja ajitahidi kufanya jambo la heri kwa mwenzake badala ya kumuumiza,” amesema katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake.
“Tuwe baraka kwa watu wengine na siyo kitunguu cha kuwatoa watu machozi,” amesema.
Mchungaji Joel Okindo, ambaye ni Msaidizi wa Mwenyekiti wa Divesheni ya Mashariki na Kati amewaka waumini kujenga moyo wa kujitolea katika masuala ya maendeleo ili kutimiza azima ya uumbaji.
Amesema ujenzi wa Kanisa la SDA – Magomeni ulianza takribani miaka 12 iliyopita na umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 kutokana na michango ya waumini, wafadhili na viongozi mbalimbali.