CCM Katavi yajibu kauli ya Arfi

Mpanda. Baada ya aliyewahi kuwa mbunge wa Mpanda Mjini mkoani Katavi, Said Arfi kusema Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatumia nguvu kubwa kuua vyama vya upinzani, chama hicho kimepinga kauli hiyo.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Mkoa wa Katavi, Theonas Kinyoto amesema tuhuma hizo si za kweli, bali vyama vya upinzani bado ni vichanga hivyo ni vyema vijipange viweze kukua na kushindana na chama hicho.

Arfi ambaye ni mwana CCM alitoa kauli hiyo hivi karibuni alipozungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Mtaa wa Madukani, Manispaa ya Mpanda.

Pamoja na mambo mengine alizungumzia kuhusu uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa akisema:

“Tumeona kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu wagombea wa upinzani walikatwa majina na wengine kuenguliwa majina yao kwenye uchaguzi jambo hili halina afya ya kidemokrasia katika nchi yetu yenye mfumo wa vyama vingi.

“Na sijui kwa nini chama changu cha CCM kinakuwa na hofu na kutumia nguvu kubwa kuua vyama vya upinzani wakati kuna mambo mengi ambayo kimefanya na tunaweza kuwaeleza wananchi na tukashinda kwa haki kuliko kuwaondoa wapinzani kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi na sijui wanafanya haya kwa masilahi ya nani,” alihoji Arfi.

Aliwaomba viongozi wa CCM waliangalie jambo hilo ili kutoa nafasi kwa vyama vya upinzani kukua na kuleta chachu ya maendeleo kwa wananchi na ustawi wa demokrasia ya vyama vingi nchini.

Akijibu tuhuma hizo, Kinyoto amelieleza Mwananchi leo Desemba 15, 2024 kuwa: “Tuhuma alizotoa mzee wetu Said Arfi siyo za kweli, kwani katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita na chaguzi zingine huwa inakuwa ni mchakato kwa kila chama kujiandaa kwa ajili ya kupata viongozi bora ambao watashindana na vyama vingine. Hilo sisi cha chama tawala tulilifanya na tukafanikiwa kupata viongozi wazuri kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na ndiyo maana tulishinda kwa kishindo,” amesema.

Amesema mkoani Katavi vyama vyote vilipewa utaratibu wa kufanya kwenye uchaguzi lakini cha kushangaa vingine kuna maeneo havikusimamisha wagombea, badala yake wa CCM walipigiwa kura ya Ndiyo na Hapana.

“Sasa inakuwaje tunaambiwa tunatumia nguvu kuua upinzani? Tulishirikishwa vyama vyote na kufahamishwa kanuni na taratibu zote za uchaguzi, ndiyo maana walishiriki uchaguzi kwa kiwango walichoweza,’’ amesema.

Amesema CCM ina malengo mengi lakini kuu katika uchaguzi wowote ni kuchukua dola, ndiyo maana ikifika kipindi cha uchaguzi husimama imara zaidi kuliko kipindi kingine chochote ili kutimiza katiba na malengo ya chama hicho.

“Sijui vyama vingine malengo yao ni yapi ndiyo maana utakuta vyama havijasimamisha wagombea baadhi ya maeneo na maeneo waliyoweka wagombea unakuta hakuna mawakala wa kuhesabu kura. Upungufu huu  ndiyo unasababisha baadhi ya watu na wazee wetu hao kusema CCM kinakandamiza upinzani jambo ambalo siyo la kweli,” amesema.

Amesema huenda Arfi amesahau wakati wa mchakato wa uchaguzi ulipoanza kulikuwa na utaratibu wa wananchi kujiandikisha kwenye daftari la mkazi na vyama vyote vilishiriki kuhamasisha wanachama na wananchi kwa ujumla kujiandikisha ili wapate nafasi ya kuchagua na kuchaguliwa.

“Tukiachana na uchaguzi wa serikali za mitaa (wa Novemba 27, 2024) ambao ndio umeleta malalamiko haya, vyama vya upinzani vimepewa nafasi ya kufanya mikutano ya hadhara mpaka sasa hawajafanya jambo lolote kama chama cha siasa.

“Ninachotaka kusema wasitafute mchawi wakati wachawi ni wao wenyewe wanatakiwa kujipanga, kuangalia walipojikwaa na kuweka mikakati vizuri itakayowasaidia kufikia malengo yao,  lakini si kulaumu na kulalamika kwa kusingizia chama chetu tawala CCM kuwa kinaminya vyama vya upinzani visikue,” amesema.

Related Posts