Morogoro/Dar. Kijana wa jamii ya wafugaji, Jisandu Mihayo (19), mkazi wa Kijiji cha Chiwangawanga wilayani Ulanga amefariki dunia, ikidaiwa alipigwa fimbo kichwani na mwenzake walipokuwa wakicheza.
Inadaiwa alikuwa akicheza na wenzake michezo ya jadi ya kushindana kuchapana fimbo mwilini.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jumapili, Desemba 15, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama kijana huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia leo alipokuwa akipatiwa matibabu kituo cha afya Mwaya, wilayani Ulanga.
Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha akiwa na vijana wenzake walikuwa wakicheza michezo ya jadi wakishindana kuchapana fimbo, huku wengine wakishangilia.
Kamanda Mkama amesema Mihayo alichapwa fimbo kichwani na mwenzake ambaye hajafahamika jina, kisha akaanguka na kupoteza fahamu.
“Baada ya kuangua na kupoteza fahamu wasamaria wema walimpeleka kituo cha afya Mwaya. Hata hivyo, alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu,” amesema.
Kamanda huyo amesema uchunguzi unafanyika kuangalia kwa ujumla mazingira ya tukio na wa kidaktari kwa mwili wa marehemu.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka mtuhumiwa wa mauaji hayo wakati hatua za uchunguzi zikiendelea kukamilishwa ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Kamanda Mkama ametoa tahadhari kwa vijana kuepuka michezo yenye kuhusisha silaha inayoweza kusababisha maradhi kimwili na hata kifo.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi linachunguza kifo cha Ayoub Ibrahimu (35), aliyefariki dunia kwa kupigwa risasi, ikidaiwa alikuwa kwenye harakati na wenzake za kuiba betri za taa za barabarani, mali ya Serikali.
Ayoub, mkazi wa Mkalama wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro imeelezwa amefariki dunia akiwa njiani akipelekwa hospitali kwa matibabu baada ya kupigwa risasi.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimajaro, Simon Maigwa imeeleza tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Desemba15, 2024 saa nane usiku.
“Tukio limetokea katika eneo la Manispaa ya Moshi, Kata ya Mawenzi, Tarafa ya Moshi Mashariki marehemu akiwa na mwenzake wakiwa katika harakati za kufungua ili kuiba betri za taa za barabarani mali ya Serikali,” amesema.
Amesema wakati wakiwa katika harakati hizo, walinzi wa manispaa wanaolinda maeneo hayo waliwaamuru wajisalimishe.
“Walipokaidi amri hiyo mlinzi alifyatua risasi hewani iliyowafanya waanze kutimua mbio. Mlinzi mmoja alifyatua risasi nyingine ambayo ilimpiga Ayoub na alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa Hospitali ya Rufaa Mawenzi kwa matibabu,” amesema.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linatoa rai kwa wananchi waaminifu kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kutoa taarifa za wizi wa mali za umma kama betri za taa za barabarani, ili hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ziweze kuchukuliwa,” amesema.