Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
VURUGU kubwa ambazo zilitokea katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam wakati Timu ya Simba ikicheza na Timu ya SC Sfaxien ya Tunisia zimesababisha kung’olewa kwa viti 256.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa na Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam Jumanne Muliro amesema viti ambavyo vimeng’olewa wakati wa vurugu hizo viti vya rangi ya blue 156 na Orange 100.
“Uwanja wa Benjamin William Mkapa Temeke Dar es Salaam kwenye mchezo wa mpira wa miguu wa kimataifa wa kombe la Shirikisho Afrika kati ya timu ya Simba ya Tanzania na CS SFAXIEN ya Tunisia kulitokea fujo…
“Iliyosababishwa na mashabiki wa timu ya CS SFAXIEN kutoridhika na maamuzi ya refa wa mchezo huo kuchezesha mechi hiyo kwa zaidi ya dakika saba ambazo aliziongeza kama dakika za nyongeza jambo lililopelekea timu ya Simba kupata goli la pili na la ushindi.
“Wachezaji wa ndani ya uwanja na “benchi” la ufundi la timu ya CS SFAXIEN walikasirika, wakamfuata mwamuzi wa mchezo na kuanza kufanya vitendo vyakumshambulia,”amesema Kamanda Muliro kupitia taatifa yake kwa vyombo vya habari.
Aidha amesema katika fujo hizo shabiki mmoja wa timu ya CS SFAXIEN aliumia na kupatiwa huduma ya kwanza na kuruhusiwa, huku viti vya rangi ya blue 156 na Orange 100 viling’olewa na mashabiki hao.
Ameweka wazi kuwa Jeshi la Polisi litashirikiana na mamlaka zingine za kisheria na soka kuona hatua za kuchukua dhidi ya vitendo hivyo ambavyo havikubaliki.