Simba kuwajibika kung’olewa viti kwa Mkapa

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamaganda Kabudi amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuwaandikia barua klabu ya Simba kuhusu ung’olewaji wa viti uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jana.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini wa Wizara hiyo, imesema barua hiyo itakayoelekezwa kwa Simba iwanakiri na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili gharama za uharibifu huo zilipwe.

Vurugu ziliibuka jana Desemba 15, 2024 katika mechi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baina ya Simba dhidi ya CS Sfaxien, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

“Vitendo vilivyofanyika jana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa havikubaliki na sio vya kimichezo, nakuelekeza Katibu Mkuu kuchukua hatua mara moja. Pamoja na kuwaandikia Simba Sports Club na TFF, wapeni ushirikiano Polisi ili watu wote waliokuwa wanang’oa viti na kuvitupa wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria, lazima tabia hii ikomeshwe” amesema Profesa Kabudi

Waziri Kabudi amewataka mashabiki wanaoingia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuacha vitendo vya uharibifu wa uwanja kwa kuwa wanasababisha hasara kwa Serikali na kuharibu ubora wa uwanja.

Baada ya vurugu hizo kutokea, jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema viti 256 viling’olewa katika vurugu hizo.

“Kulitokea fujo iliyosababishwa na mashabiki wa Timu ya CS Sfaxien kutoridhika na maamuzi ya refa wa mchezo huo kuchezesha mechi hiyo kwa zaidi ya dakika saba ambazo aliziongeza kama dakika za nyongeza jambo lililopelekea timu ya Simba kupata goli la pili na la ushindi.

Wachezaji wa ndani ya uwanja na “benchi” la ufundi la timu ya CS Sfaxien walikasirika, wakamfuata mwamuzi wa mchezo na kuanza kufanya vitendo vya kumshambulia.” imesema taarifa hiyo ya polisi

Hata hivyo shabiki mmoja wa timu ya CS Sfaxien alidaiwa kuumia na kupatiwa huduma ya kwanza na kuruhusiwa, huku viti vya rangi ya bluu 156 na machungwa 100 viling’olewa na mashabiki.

Related Posts