Chikola: Miamala ilisoma kisa Yanga

Katika Ligi Kuu Bara msimu huu mpaka sasa huenda ushindi wa mabao 3-1 wa Tabora United mbele ya Yanga katika Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam ndiyo matokeo ya soka ambayo yamezungumzwa zaidi, kuzua mijadala, hisia tofauti na maamuzi ya kushangaza.

Matokeo hayo yasiyo ya kutegemewa wakati yakishusha furaha na shangwe kubwa mkoani Tabora huko Jangwani yaliacha kilio kwa uongozi wa Yanga kumtupi virago Kocha Miguel Gamondi na msaidizi wake, Mussa N’daw.

Nyuma ya matokeo hayo kuna shujaa wa Tabora United, winga Offen Chikola aliyefunga mabao mawili kwenye mchezo huo na kuteka hisia za mashabiki, huku akifunga tena dhidi ya KMC ambapo katika michezo hiyo miwili aliibuka nyota wa mchezo.

Mwananchi limezungumza kwa kina na Chikola aliyefunguka mambo mengi ikiwemo namna ambavyo Yanga imebeba historia kubwa katika safari yake ya soka.

Chikola anasema mechi yake ya kwanza Ligi Kuu Bara msimu wa mwaka 2016/2017 akiwa Ndanda FC ni dhidi ya Yanga katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam Septemba 23, 2017 ambao ulimalizika kwa Yanga kushinda bao 1-0, lililofungwa na Ibrahim Ajibu.

Anasema akiwa amesajiliwa Ndanda FC kama mchezaji wa timu ya U-20, msimu ulianza kwa kusugua benchi katika mechi tano za kwanza lakini mchezo wa sita dhidi ya Yanga akapewa nafasi na kocha Malale Hamsini aliyemtaka akamdhibiti Juma Abdul asipandishe mashambulizi.

“Kipindi cha pili kilipoanza kocha aliniita akaniambia sasa nakupa nafasi mwanangu nikashangaa mechi yangu ya kwanza ndio nacheza na Yanga sijawahi kugusa hata mechi yoyote ya ligi nikaona kama kocha ananiletea masihara,” alisema Chikola na kuongeza;

“Akaniambia ondoa presha yote mwanangu mimi ndiye kocha nimekuamini nakupa nafasi najua hii ni mechi yako ya kwanza nakupa maelekezo kayafanye lakini unachoona unaweza kukifanya kwenye timu kifanye lakini kwa kuzingatia maelekezo yangu,” alisema.

Alisema licha ya kuwa na hofu lakini alizingatia maelekezo ya kocha na kutuliza presha kwa kuhakikisha mipira miwili ya kwanza hakosei jambo lililomsaidia kuingia kwenye mfumo wa mchezo na kucheza vizuri na kumridhisha kocha  aliyemuanzisha katika mechi zote zilizofuata.

Historia yake na Yanga haikuishia hapo kwani msimu wa mwaka 2021/2022 akiwa na Geita Gold kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Yanga uliopigwa Aprili 10, 2022 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Chikola aliitanguliza timu yake dakika ya 87 kabla ya Juma Shaban kusawazisha dakika ya 90 kwa penalti na mchezo huo kumalizika kwa sare ya 1-1 kabla ya Yanga kusonga mbele kwa mikwaju ya penalti 7-6.

Winga huyo anasema mabao mawili aliyoifunga Yanga yalifanya apigiwe simu nyingi ambazo hajawahi kuzipata huko nyuma huku akishangazwa na namna ambavyo mashabiki wa Yanga walimpokea vizuri bila kumtukana au kumtishia maisha kama ilivyozoeleka.

“Nimepokea pongezi nyingi, nimepigiwa simu nyingi kwa watu wa mpira wakinipa hongera kwamba nimefanya kitu kizuri, kuniambia niongeze juhudi na waliokuwa wanaweza kukupa chochote kitu walinipa,” alisema Chikola.

“Baada ya mechi kuisha nilikuwa upande wa mashabiki wa Yanga nilidhani watanizomea lakini waliniita wakataka tupige picha na kunipongeza kwa kazi nzuri ni jambo ambalo nilifurahishwa nalo na kujisikia vizuri.”

Alisema pongezi hizo hazikuishia hapo kwani hata nje ya uwanja kwenye maisha ya kawaida mtaani, ndugu, marafiki na jamaa walipiga simu licha ya kuumizwa na matokeo lakini walifurahi kwa kuwa aliyefanya ni kijana wao.

Nyota huyo anasema furaha iliyoonyeshwa na mashabiki, uongozi wa timu, mkoa na wadau mbalimbali ni deni kwa wachezaji kuhakikisha wanaendelea kukidhi matamanio ya mashabiki hao ambao kwa sasa wamehamasika na timu yao.

“Kilichotokea ni mpango wa Mungu lakini ni kitu ambacho sasa tunadaiwa na watu kwa sababu watakuwa wana imani kubwa na sisi hasa mashabiki wa hii timu, tunachopaswa sasa ni kupambana na kutafuta ushindi kila mechi,” alisema Chikola.

Chikola anasema kinachofanywa na Tabora United kwenye ligi siyo cha kubahatisha kwani ni matokeo ya usajili mzuri na wa maana uliofanyika dirisha kubwa ukihusisha wachezaji bora na wazoefu wa mashindano makubwa akiwemo Yacouba Songne, Salum Chuku na Haritier Makambo.

“Viongozi wamejitahidi kusajili wachezaji wazuri ukiangalia timu yetu imekamilika makipa wazuri, mabeki wa kati bora na wazoefu mpaka safu ya mbele akina Makambo na Yacouba wazoefu na wameshacheza nchini, kwao Congo na kimataifa,” alisema winga huyo.

Licha ya kuanza vizuri Ndanda na kuaminiwa na kocha Malale Hamsini akiwa na umri chini ya miaka 20 tu, safari ya winga huyo kikosini hapo iliingia dosari na kupoteza mwelekeo wake kwenye soka baada ya ujio wa Mrisho Ngassa kutoka Mbeya City.

Anasema usajili wa Ngassa dirisha dogo ulitokana na presha ya viongozi ambao hawakuwa na imani naye kutokana na uchanga wake kwenye ligi na kumtaka ampishe Ngassa na kuendelea kujifunza kwake.

“Waliniambia wewe bado mdogo endelea kukaa pembeni ujifunze kwa wakubwa nilikubali na niliamini nitajifunza mengi ambacho mimi nilishindwa na bahati nzuri Ngassa alifanya vizuri kuanzia hapo sikupata kabisa nafasi mpaka mzunguko wa pili unaisha,” alisema Chikola.

“Msimu uliofuata nilitegemea ndiyo ungekuwa wa kufanya makubwa kwangu lakini wakati tukiwa mapumziko wakati dirisha linakaribia kufungwa kikosi cha msimu mpya kilivyotoka jina langu halikuwemo.

“Nilimuuliza kocha akadai nimo lakini viongozi wakagoma kupokea simu zangu dirisha likafungwa nikakosa timu ikabidi nikae nje miezi sita bila kucheza kikawa kipindi kigumu sana kwangu.”

Anasema hakukata tamaa kwani dirisha dogo alijiunga na Mawenzi Market iliyokuwa daraja la kwanza (sasa Championship) kwa mkataba wa miezi sita na kudumu kwa msimu mmoja na nusu jambo lililomsaidia kurejesha makali yake.

Baada ya hapo alisajiliwa na Fountain Gate iliyokuwa daraja la kwanza na kisha kusajiliwa na Geita Gold baada ya kupanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2020/2021 ambapo amedumu nayo kwa misimu mitatu hadi 2023/2024 iliposhuka daraja na kutimkia Tabora United.

Related Posts