Kitendo cha kikundi cha mashabiki wa CS Sfaxien kupeperusha bendera za Palestina katika mechi yao dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa huenda kikaiponza timu hiyo.
Kwa mujibu wa ibara ya 49 ya katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), hairuhusiwi uonyeshwaji wa jumbe zenye mlengo wa kisiasa katika eneo kunakofanyika tukio la kimashindano.
“Hakuna uonyeshwaji wowote wa kisiasa, kidini au propaganda za kibaguzi ambao unaruhusiwa katika eneo la kimashindano la Caf,” inafafanua ibara hiyo.
Katika mchezo wa Simba na Sfaxien, mashabiki wa timu hiyo ya Tunisia wameonekana wakipeperusha bendera za nchi ya Palestina.
Muda wa mapumziko, walitembeza bendera kubwa ya nchi hiyo katika jukwaa la upande wa Kaskazini ambako walikuwa wamekaa.
Wakati wakifanya hivyo, ofisa habari wa Caf kwenye mechi hiyo, Ahmed Hussein kutoka Uganda ameonekana akipiga picha kwa simu yake ya mkononi tukio la mashabiki hao kupeperusha bendera hizo, ikionekana kama kuchukua ushahidi wa jambo hilo.