Kipyenga chalia Chadema, Mnyika awaonya wagombea

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimefungua pazia la uchukuaji na urejeshaji fomu za uchaguzi wa viongozi wa wakuu wa cha hicho ngazi ya Taifa na mabaraza yake.

Hatua hiyo inakwenda kuongeza joto la uchaguzi ndani ya Chadema, ambapo tayari makamu mwenyekiti wake-Bara, Tundu Lissu ametangaza nia ya kuwania nafasi ya uenyekiti.

Kwa sasa nafasi hiyo inashikiliwa na Freeman Mbowe, ambaye bado hajaweka wazi iwapo atajitosa kutetea nafasi hiyo.

Tayari minyukano inaendelea kushika kasi ndani ya Chadema kutokana na joto la uchaguzi huo, huku wanachama wakianza kujigawa makundi, kuwapambania wagombea wanaowataka kushinda.

Kipyenga cha uchukuaji fomu kwa ajili ya uchaguzi huo utaanza kesho Jumanne, Desemba 17, 2024 mpaka Januari 5, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Desemba 16, 2024, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema nafasi zitakazowaniwa ni Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti (Bara na Zanzibar) pamoja na mabaraza yote ngazi ya Taifa, huku mkutano mkuu ukipangwa kufanyika Januari 21, 2025 baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa Baraza la Vijana Taifa Chadema (Bavicha), Baraza la Wazee Chadema (Bazecha) na Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha).

“Fomu zitaanza kutolewa kesho (Desemba 17, 2024) na gharama zake zinazingatia hali halisi ya kimaisha na mara ya mwisho zilipitiwa kwenye mkutano mkuu mwaka 2019 na havijabadilishwa. Wagombea wote wanaotaka kuwania nafasi hizo wanakaribishwa kuchukua fomu.

“Kwa mabaraza ya vijana, wanawake na wazee watatakiwa kurejesha fomu kwenye ofisi za mabaraza zilizopo Mtaa wa Ufipa, jijini Dar es Salaam ama kwenye ofisi za kanda anakotoka mgombea husika,” Amesema Mnyika na kuongeza:

“Gharama ya fomu itategemea na nafasi anayogombea na atatakiwa kuambatanisha risiti ya malipo yaliyotumwa kwenye akaunti ya chama.”

Kwa mujibu wa Mnyika, gharama za uchukuaji fomu kwa nafasi zinazowaniwa Mwenyekiti wa Taifa ni Sh1.5 milioni, makamu mwenyekiti Sh750,000.

Kwa upande wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema ambao ni wanane kutoka pande zote, gharama ya fomu ni Sh300,000.

Gharama kwa Bazecha, Bawacha

Mnyika ambaye amewahi kuwa mbunge wa Kibamba, amesema fomu ya mwenyekiti wa Bazecha ni Sh300,000, makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar ni Sh150,000.

“Kwa Katibu Mkuu Bazecha fomu itakuwa Sh 150,000 sawa na manaibu wake kutoka Bara na Zanzibar fomu ni Sh 150,000 sawa na mweka hazina, huku wajumbe wanne gharama ya fomu ni Sh100,000. Wajumbe 20 wa mkutano mkuu gharama za fomu itakuwa Sh50,000,” amesema Mnyika

Kwa upande wa Bawacha, gharama ya fomu kwa mwenyekiti Taifa itakuwa Sh300,000, makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar ni Sh150,000 sawa ilivyo kwa katibu mkuu.

Wakati kipyenga cha uchukuaji fomu kikipulizwa, Mnyika ametoa angalizo kwa wagombea wote kuhakikisha wanazingatia katiba, kanuni na maadili ya chama.

Amesema Chadema kina miongozo yake ya uendeshaji wa kampeni ndani ya chama.

“Wanachama na wagombea wote wanapaswa kuzingatia na kufuata muongozo wa chama dhidi ya rushwa kama inavyoeleza katika toleo la mwaka 2012,” amesema Mnyika.

Related Posts