Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda ameitaka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kuongeza uwazi kwenye mchakato wa upangaji mikopo na vigezo, ili kuondoa malalamiko ambayo wakati mwingine yanasababishwa na makosa yanayofanywa na waombaji.
Profesa Mkenda amesema malalamiko mengi ya wanaokosa mikopo au udahili katika taasisi za elimu ya juu ni matokeo ya waombaji kutokamilisha taarifa zinazohitajika kwenye maombi, hivyo kujikuta wakishindwa kukidhi vigezo.
Amesema hayo leo Jumatatu, Desemba 16, 2024 jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa programu rununu (app) ya HESLB.
Profesa Mkenda amesema malalamiko mengi ya watu kukosa mikopo na udahili vyuoni ni matokeo ya kutokamilisha taarifa na wengine kutoweka taarifa sahihi.
“Suala hili ningeomba wazazi na wanafunzi walifahamu vyema, kuna malalamiko mengi lakini ukweli ni kwamba, sababu mojawapo ya kukosa mkopo ni kutokamilika kwa taarifa.
“Usipoweka taarifa sahihi upo uwezekano mkubwa wa kukosa mkopo na kupangiwa kozi. Hili tunaliona na nimeshakutana na kesi za aina hii, mtoto analalamika amepangiwa kozi ambayo hakutaka nilipofuatilia hakujaza mwenyewe alijaziwa,” amesema.
Ili kukabiliana na hilo, amesema ni muhimu kwa taasisi zinazohusika na elimu kuweka wazi mifumo yake kurahisisha watu wenye malalamiko kuingia na kujiridhisha katika kile wanachokilalamikia.
“Licha ya kazi nzuri mnayoendelea kuifanya ningeomba HESLB kuwa wawazi, watu waone vigezo na mchakato wa upangaji, hii itaondoa malalamiko maana napokea mengi na ukifuatilia unagundua kuna makosa yalifanyika.
“Nitoe rai kwa wananchi, kupeleka malalamiko kwa viongozi haiwezi kusaidia kama hukuwasilisha taarifa sahihi kwenye uombaji. Hakikisha unajaza na unatoa taarifa sahihi na kamilifu,” amesema.
Hii si mara ya kwanza kwa suala hilo kuzungumzwa, Agosti mosi, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia akizungumzia siku 60 tangu kufunguliwa kwa dirisha, alisema wamebaini kuna maombi hayakamiliki kwa sababu yanatumwa na watu wasio sahihi.
Dk Kiwia aliwataka wazazi kuacha kuwajazia fomu za maombi watoto wao kwa kile alichoeleza wengi hawana taarifa muhimu zinazohitajika, hivyo kusababisha maombi kutokamilika.
“Inawezekana mzazi anafanya kwa nia njema kabisa kumuombea mtoto wake mkopo, kinachotokea kuna taarifa ambazo anaweza asiwe nazo na hii inasababisha maombi yasikamilike na akamkosesha fursa hiyo,” amesema.
Aliwataka wazazi kuwawezesha watoto kufikia huduma za mtandao, ili waweze kutuma maombi lakini wawaache wajaze wenyewe fomu kwa kuwa ndio wenye taarifa sahihi.
Akizungumzia aplikesheni hiyo, Dk Kiwia amesema itasogeza karibu huduma za bodi ya mikopo na itahusisha pia wanaoirejesha.
Amesema uwekezaji uliofanyika kwenye Tehama kuanzia mwaka 2015 hadi sasa umewezesha huduma za bodi kuwa za kidijitali kwa asilimia 90.
Amesema kuanza kazi kwa app hiyo kutazifanya huduma hizo kuwa za kidijitali kwa asilimia 100.
“Hadi 2024 asilimia 90 ya shughuli za bodi zinafanyika kwenye mfumo. Katika kufikia asilimia 100 tumekuja na app ili iweze kutekeleza dhana nzima ya taasisi hii kutotumia karatasi.
“App itawasadia pia wanufaika wa mikopo kwa sababu watapata fursa ya kujisajili kidijitali na kuwezesha kupata malipo yao kidijitali. Wanufaika wa mikopo wanaweza kuona taarifa zinazohusu upangaji na urejeshaji wa mikopo,” amesema.
Amesema: “Mfumo huu huko mbeleni utaendelea na kumfuatilia mwanafunzi aliyemaliza chuo kupitia portal maalumu tutakayoweka na kushirikiana na wadau wengine kuweka fursa za ajira. Wito kwa wanafunzi kujisajili kwenye app ili waweze kupokea malipo yao kwa njia ya kidijitali kwa wepesi na haraka.”