Mwanza. Huenda ukawa ni miongoni mwa watu wanaotarajia kusafiri mwishoni mwa mwaka kwenda kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya.
Jeshi la Polisi limetaja mambo saba ya kufuatwa na madereva, abiria na watumiaji wa barabara ili kuepuka ajali za barabarani katika kipindi hicho.
Mambo hayo yametajwa leo Jumatatu, Desemba 16, 2024 na Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma na Mafunzo ya Usalama Barabarani, Michael Deleli alipozungumza na madereva, abiria na mawakala wa magari katika stendi kuu ya mabasi ya Nyegezi, jijini Mwanza.
Deleli amesema ili kuepusha ajali kutokea, madereva wanapaswa kuepuka mwendokasi, ulevi, kutowapuuza watumiaji wengine wa barabara, kupata mapumziko ya kutosha kabla ya kuanza safari na kuhakikisha wanafuata sheria wanapoendesha vyombo vya usafiri barabarani.
Amewataka madereva kuepuka tabia aliyoiita ya ‘kenge’ akimaanisha kukurupuka wanapokuwa barabarani, akisema ajali nyingi hutokea madereva wanapokurupuka ku- overtake (kuyapita) magari mengine barabarani.
Mbali ya hayo, amewataka wasio na uzoefu kutafuta madereva wa kuendesha magari yao.
Deleli amewataka abiria kutochochea madereva kuendesha kwa mwendokasi jambo alilosema linaweza kumkosesha utulivu barabarani, mawakala kutoongeza nauli kiholela, watembea kwa miguu kutumia maeneo yaliyoelekezwa barabarani na wenye tabia ya kushambulia magari kwa mawe kuacha kufanya hivyo.
“Uzoefu unaonyesha ajali nyingi zinatokea kwa sababu ya madereva, abiria au watumiaji wengine wa barabara kutozingatia mambo hayo.
“Juzi imetokea ajali Singida na kuua wanne, uchunguzi wa awali ulibaini dereva alikuwa amechoka, tunasisitiza kuzingatia hayo,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, Sunday Ibrahim amewataka madereva wa vyombo vya moto kutoshtuka watakapoona utitiri wa trafiki barabarani kwa kile alichoeleza maofisa hao wanalenga kukomesha ajali.
Amesema doria za barabarani zinaendelea mkoani humo usiku na mchana, kwa lengo la kuhakikisha hakuna dereva anayevunja sheria na kusababisha ajali inayoweza kugharimu afya au uhai wa wananchi wengine.
“Tumepokea maelekezo ya Afande Deleli na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa na tayari tumesambaza askari wetu mitaani kuhakikisha sheria ya usalama barabarani inazingitwa na hakuna mwananchi anayepata madhara anapokwenda kusherehekea sikukuu,” amesema.
Dereva wa basi la kampuni ya Isamilo, Emmanuel Mnyaga mbali ya kuomba kupunguzwa vizuizi vya askari barabarani, ameliomba jeshi hilo kuwachukua hatua kwa abiria wenye tabia ya kushambulia magari yanapopita akisema vitendo hivyo pia husababisha ajali.
Maryene Munuo, ambaye ni abiria amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kutoa elimu akiomba iwe endelevu.
“Tunaahidi kutoa ushirikiano kwa polisi tukibaini kuna ukiukwaji wa sheria, mfano dereva akiendesha mwendokasi tutatoa taarifa,” amesema.
Abiria katika basi la Zuberi linaloelekea mkoani Arusha, Elex Mongi amesema abiria ni miongoni mwa sababu za ajali kwa kuchochea mwendokasi, akiahidi kukemea tabia hiyo na ukiukwaji wa sheria ya usalama barabarani.