Unguja. Licha ya mafanikio ya Taasisi ya Ofisi ya Rais, Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (ZPDB), wapo baadhi ya watendaji wanatajwa kukwamisha utendaji wa taasisi hiyo na kushindwa kutoa ushirikiano.
Hayo yameelezwa leo Desemba 16, 2024 Ikulu Zanzibar na Mtendaji Mkuu wa ZPDB, Profesa Mohamed Khalfan alipotoa taarifa kwa Rais Hussein Mwinyi, katika maadhimisho ya miaka miwili tangu kuundwa kwa taasisi hiyo.
“Siyo vizuri kuanika nguo chafu hadharani lakini hili lazima niliseme, pamoja na kutamka kwako zaidi ya mara moja kuwa ZPDB ni taasisi yako na utendaji wake ni sehemu ya kutekeleza maagizo na vipaumbele ambayo unavisimamia, bado baadhi ya viongozi hujaribu kuingilia utendaji wetu na kusababisha kuchelewesha matokeo ya haraka kwa wananchi.
“Kwa uwazi kabisa hili halitupendezi na kwa heshima na unyenyekevu, tunaomba kukumbusha kuwa mtendaji mkuu wa ZPDB anapaswa kuripoti kwa Rais,” amesema.
Amesema baadhi ya watendaji wa Serikali wanaichukulia taasisi hiyo kuwa ipo kwa ajili ya utafutaji makosa, hivyo hukataa kutoa ushirikiano.
Hata hivyo, amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika miradi ya sekta za elimu, afya, miundombinu, bado taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto zikiwemo za vitendea kazi.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wakuu wa taasisi za Serikali, Rais Mwinyi amesema amepokea changamoto zilizowasilishwa na atazifanyia kazi kuleta ufanisi zaidi ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.
Amesema lengo ni kuhakikisha mipango ya Serikali inasimamiwa vyema katika utekelezaji na wameona matunda tangu kuundwa kwa taasisi hiyo.
“Niliposhika madaraka mwaka 2020 nilitafuta njia za kunisaidia katika utekelezaji wa shughuli za Serikali nikaona kuna njia nyingi lakini moja ni kuanzisha taasisi yenye kazi ya kufuatilia, kusimamia na kutekeleza mipango tuliyoipanga,” amesema.
Ameipongeza taasisi hiyo akisema bila nguvu yao mengi yangekuwa bado yanasuasua.
“Bado ipo kazi ya kufanya, nitaendelea kukaa nao kuwapa maelekezo ili tuondokane na ile tabia iliyojengeka ndani ya vyombo vya Serikali kwa miaka mingi ya kufanya kazi kwa mazoea ya kutokuwa na haraka, jambo la kuchukua miaka mitatu hadi mitano kwa kazi inayoweza kufanyika kwa miezi sita.”
“Bado tuna kazi ya kufanya lakini hapa tulipofika si haba, tumesukumana mpaka kufikia hapa, kazi iliyopo mbele yetu ni kubwa zaidi,” amesema.
Amesema taasisi kama hizo siyo ngeni duniani ambazo zinaundwa kwa dhamira ya kuleta usimamizi wa utendaji.
Amesisitiza timu za wataalamu ziendelezwe na kujengewa uwezo kufanikisha vipaumbele vya Serikali kwani utekelezaji wake unaleta matokeo chanya kwa vitendo.
“Ni muhimu kuendelea kuwepo ushirikiano wa karibu kati ya taasisi hiyo na Serikali,” amesema.
Dk Hussein Mwinyi alipozindua taasisi hiyo Desemba 2022 alitaja vipaumbele ni katika sekta za miundombinu, utalii, uchumi wa buluu na huduma za jamii. Amesema viashiria alivyotoa hadi kufikia Desemba 2024 vinaonyesha kufikiwa japo si kwa asilimia 100.
Kuhusu matumizi ya mfumo wa kidijitali kwa njia ya Dashboard, Dk Mwinyi amesema itarahisisha na kuleta ufanisi katika ufanyaji kazi na kutathmini miradi yote ya maendeleo.
Amesema sekta zote zitatumia mfumo huo kikamilifu katika utoaji wa taarifa za miradi ya vipaumbele.
Ameahidi kuwapa nyenzo na bajeti ya kutosha kuhakikisha wanashirikiana kukabiliana na changamoto zinazopunguza kasi ya kutekeleza majukumu yao.
Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Godffrey Nyamrunda amesema wamekuwa wakishirikiana na taasisi hiyo katika utendaji, hivyo wataendelea kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanyika Zanzibar.
Mwakilishi wa Taasisi ya Tony Blair (TBI), Layla Ghaid amesema mabadiliko yanatumia muda mrefu lakini wataendelea kuimarisha uratibu wa kazi ili kuleta ufanisi zaidi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Kwa mwaka mwingine tunaahidi kuendeleza taratibu za utekelezaji wa miradi, kufanya tathmini na kuisaidia Serikali kuonyesha athari chanya zinazopatikana katika utekelezaji wa miradi hiyo.