Nyumba za Gachagua zinavyolindwa na wanajeshi wa kujitolea

Nairobi. Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amesema nyumba zake za Nairobi na Mathira huko Nyeri sasa zinalindwa na askari wa kujitolea, baada ya Serikali ya Rais William Ruto kuondoa walinzi wake.

Gachagua amesema askari hao wa kujitolea wanajumuisha wanaume na wanawake waliowahi kuhudumu katika Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Jeshi la Huduma ya Polisi, Wakala wa Wanyamapori Kenya na Wakala wa Misitu Kenya.

“Rais Ruto alipoamuru kwamba ulinzi wangu uondolewe baada ya kuzomewa katika Kaunti ya Embu wakati mimi nikishangiliwa, watu wengi wa jamii yangu walipata wasiwasi,” amesema wakati wa mahojiano na Inooro TV Jumapili jioni.

Ameongeza kuwa: “Watu wengi walikuwa na wasiwasi kuhusu usalama wangu niliposhambuliwa huko Limuru na nia ilikuwa kuniua.”

Gachagua ameeleza kwamba alipata ofa hiyo kutoka kwa watu wenye nia njema ambao waliwahi kuhudumu kwenye vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya, huku akiwaita ni wazalendo waliojitolea kutoka katika jamii yake.

“Kwa sasa nyumba zangu na mimi mwenyewe tuko chini ya ulinzi kutoka kwa wale wanaojitolea…takribani 300…sasa niko sawa, nimestarehe na sihitaji ulinzi wa Serikali,” amesema.

Ulinzi wa Gachagua uliondolewa mwishoni mwa Novemba baada ya kushtakiwa kufadhili upinzani dhidi ya Serikali ya Rais Ruto.

Hayo yanajiri wakati duru za siri katika Wizara ya Mambo ya Ndani zikiiambia Nation kuwa “mamlaka za juu katika nchi hii zinataka Gachagua azuiwe kuiingiza nchi katika kampeni za mapema, ili Serikali itekeleze miradi ya maendeleo.

“Hapa tuna mtu ambaye tulimshauri kwa busara ajiuzulu badala ya kungoja kushtakiwa. Tulikuwa tumemhakikishia kwamba atapata ulinzi, bajeti, marupurupu yake na kurahisishwa kuendelea na mpango wa siasa kabla ya 2027,” kimeeleza chanzo kimoja kutoka katika wizara hiyo.

Kuondolewa kwa ulinzi kwake kulifanyika, licha ya agizo la Mahakama kutaka serikali kutoingilia mpango wa ulinzi wa makamu huyo wa Rais wa zamani hadi kesi yake itakaposilikizwa na kuamuliwa.

Gachagua ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Mathira, alimlaumu Rais Ruto na Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja kwa shambulizi la Novemba 28, 2024 dhidi yake huko Limuru.

Gachagua alikuwa akihudhuria mazishi ya Erastus Nduati katika kijiji cha Bibirioni, kundi la vijana lilimvamia na kulazimisha walinzi wake kumwokoa.

Gari lake binafsi liliharibiwa kwa kiasi kikubwa na mmoja wa wasaidizi wake alijeruhiwa na amelazwa hospitalini hadi sasa.

Alidai shambulizi hilo lilipangwa na serikali, akisema ndiyo sababu iliyofanya hadi zaidi ya wiki mbili sasa, hakuna mtu yoyote aliyekamatwa kwa kuhusika katika tukio hilo.

“Washambuliaji walikuwa wakizungumza kwa lugha ya Gikuyu na walikuwa wakitangaza kwa sauti kwamba walikuwa wamehakikishiwa kwamba sikuwa na ulinzi wa silaha wa kunilinda.

“Walionivamia wanajulikana, sura zao ziko kwenye mitandao ya kijamii baada ya ubaya wao kurekodiwa kwenye video, ni watu wenye rekodi za uhalifu na wanajulikana, lakini bado wanaendelea kuwa huru kwa sababu serikali iliwafadhili kunishambulia.,” alisema.

Iwapo atauawa, Gachagua alinukuliwa akisema: “Rais Ruto ndiye anafaa kuwajibishwa moja kwa moja”.

Related Posts