Kaimu Naibu kamishna Idara ya Walipa Kodi wa Kati kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Godwin Barongo akimkabidhi zawadi Mwakilishi wa Kampuni ya CRJE Estate Ltd, Johari Rotana Hotel, Doris Zeng leo Novemba 16, 2024 wakati walipowatembelea ofisini kwao kwaajili ya kuwashukuru kama walipaji kodi.
KAIMU Naibu kamishna Idara ya Walipa Kodi wa Kati kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Godwin Barongo ametoa wito kwa walipakodi wote wa Tanzania wahakikishe kwamba wanalipa kodi zao mapema hasa mwezi huu wa Desemba kwa sababu ni mwezi ambao una sikukuu ndani yake kama za Krismasi, za kufunga mwaka na kufungua mwaka.
Hayo ameyasema leo Desemba 16, 2024 jijini Dar es Salaam wakati alipowatembelea katika ofisi za kampuni ya CRJE Estate Ltd kwaajili ya kuwashukuru na kuwasikiliza changamoto zao katika mifumo ya ulipaji kodi.
“Ni vizuri wakalipa kodi zao mapema, kuna wale walipakodi wanalipa kodi ya ongezeko la thamani ( VAT) muda wao wakulipa kodi ni Desemba 20, 2024 kwahiyo ingekuwa vizuri kabla ya tarehe hiyo wakaweza kulipa kodi zao kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa adhabu na riba.” Amesema
Amesema kuwa wiki hii na wiki iliyopita wamekuwa na zoezi mahususi kwaajili ya kuwatembelea walipakodi wao ili kuwashukuru kwa namna ambavyo tumeanza nao mwaka wa fedha wa Julai mpaka tunafikia Desemba ambayo ni nusu ya mwaka…. Tumelenga walipakodi ambao ni wamekuwa wakitoa mchango mkubwa kwenye makusanyo ya serikali.
Zoezi hili tunakwenda nalo kwa wiki nzima hii tukiwashukuru lakini pia tukisikiliza changamoto zao, Mapendekezo yao juu ya mfumo mzima wa kodi na namna shughuli za ukusanyaji wa kodi zinaendeshwa.
Zoezi hili limelenga sana katika kutoa shukurani kwa walipakodi wetu na kuwaomba ushirikiano tena kwa kipindi kingine cha miezi sita kitakacho tupeleka mpaka Juni 2025. ” Amesema Barongo
Amesema katika Idara ya Walipakodi wa kati ni zaidi ya Walipakodi 1200 ambao wanachangia katika kulipa kodi na haikuwa rahisi kuwatembelea wote kwahiyo wamewachagua wateja ki sekta kama sekta ya Utalii, sekta ya Viwanda, Sekta ya Wauzaji wa Jumla, kwahiyo tunapata wawakilishi kutoka kwenye sekta hizo.
Mwakilishi wa Kampuni ya CRJE Estate Ltd, Johari Rotana Hotel, Doris Zeng amewashukuru TRA kwa kutambua mchango wao katika ulipaji wa kodi hivyo wameahidi kuendelea kutoa kodi kwa maendeleo ya nchi.
Kaimu Naibu kamishna Idara ya Walipa Kodi wa Kati kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Godwin Barongo akimkabidhi zawadi Mhasibu Mkuu wa HJF, Gad Oneya leo Novemba 16, 2024 wakati walipowatembelea ofisini kwao kwaajili ya kuwashukuru kama walipaji kodi.
Kaimu Naibu kamishna Idara ya Walipa Kodi wa Kati kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Godwin Barongo wakwanza kushoto akizungumza leo Desemba 16, 2024 alipofika ofisi za Kampuni ya CRJE Estate Ltd, Johari Rotana Hotel kwaajili ya kuwashukuru na kusikiliza kero katika mifumo ya ulipaji kodi.
Kaimu Naibu kamishna Idara ya Walipa Kodi wa Kati kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Godwin Barongo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Desemba 16, 2024