Serikali mjini Njombe yawataka wanaofanya biashara maeneo yasiyo rasmi kutoka kwa hiari

Serikali mjini Njombe imewataka wafanyabiashara wanaofanya biashara zao kwenye maeneo yasiyo rasmi kuondoa biashara zao kwa hiari kwa kuwa serikali imetenga maeneo rafiki kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kwa ajili ya shughuli hizo.

Wito huo umetolewa na mtendaji wa kata ya Njombe mjini Enocy Lupimo kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe Kuruthum Sadick wakati wa zoezi la usafi uliokuwa ukifanyika katika mtaa wa Buguruni ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya usafi wa mazingira katika mitaa yote tisa ya kata hiyo ambapo amesema ni lazima wananchi wajenge tabia ya usafi na kuagiza wote waliotoa bidhaa sokoni na kupeleka barabarani kuondoa biashara hizo kabla hatu za kisheria hazijachukuliwa.

“Lazima tujizatiti katika swala la usafi na ninapeleka salamu stendi ya zamani,mkurugenzi ametoa vizimba soko kuu watu wanatoka wanaenda kupanga bizaa stendi,kama una shangazi anauza pale vitumbua pale waambieni watoke kwa hiari”amesema Lupimo

Simon Ngassa ni mratibu wa Chanjo halmashauri ya mji wa Njombe kwa niaba ya afisa afya ametaka wananchi kuchukua tahadhari kwa kufanya usafi ili kujikinga na maradhi yanayotokana na uchafu.

“Tuchukue tahadhari zote za usafi lakini pia watoto wapate chakula cha moto na wale wafanyabiashara yani mama lishe wanaotuhudumia hakikisheni kwenye mgahawa mna maji safi ya kunawa na sabuni ya maji sio kipande lakini pia muwaeleze wale wanaofanya biashara barabarani warudi sokoni”amesema Ngassa

Kwa upande wake Frolida Kietta mkaguzi msaidizi wa Polisi ambaye ni Polisi kata wa Njombe mjini ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuchukua tahadhari kuelekea sikuku za mwisho wa mwaka.

Nao baadhi ya wananchi wa Buguruni akiwemo Benjamin Mligo pamoja na Nickodem Waziri wameshukuru serikali ya mtaa kuwakumbusha katika swala la usafi na kuomba zoezi hilo kuwa endelevu.


Related Posts