Kipa wa Namungo raia wa DR Congo, Erick Molong amesema hafurahishwi na maisha anayoishi kikosini humo akieleza kuwa msimamo wake ni kuachana na timu hiyo ili kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine.
Hatua hiyo imekuja kufuatia nyota huyo kutokuwa na uhakika wa namba kwani tangu ametua kikosini hapo mapema msimu huu, amecheza mechi tatu dhidi ya Azam, Coastal Union na Tabora United.
Katika kikosi hicho eneo la golini, kipa wa zamani wa Mbeya City, Yanga, Simba na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Beno Kakolanya ndiye ameonekana kuwa chaguo la kwanza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Molong mwenye asili ya Angola, amesema kwa sasa anafikiria kutimka Namungo kutokana na kutokuwa na furaha katika kazi yake.
Amesema alikuja kwa wito na benchi la ufundi lililokuwa chini ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera (kwa sasa Mkurugenzi wa ufundi), lakini amekuwa hafanyi alichotarajia.
“Bado nina mkataba hadi Juni 28, 2025, lakini nafikiria nimalizane nao niondoke kupata changamoto mpya, nilikuja kufanya kazi lakini naona haiko hivyo.
“Uwezo wangu ni mkubwa, uzoefu wangu sina shaka nikicheza timu nyingi za Ligi Kuu Angola na nje, nachohitaji ni kufanya kazi kwani ndio jukumu langu,” amesema kipa huyo.
Hata hivyo, amesema pamoja na uamuzi wake huo, amevutiwa na soka la Tanzania kutokana na ushindani uliopo akieleza ikitokea timu yenye kuhitaji huduma yake watazungumza.
“Ligi ina ushindani japokuwa Simba, Yanga na Azam zinaonekana kuibeba zaidi Tanzania, nimevutiwa na soka lake na ikitokea timu kunihitaji tutaongea, kazi yangu ni mpira,” amesema kipa Molong.
Akizungumzia msimamo wa nyota huyo, Meneja wa Namungo FC, Idrisa Bandari amesema uamuzi wake hawawezi kuuingilia, huku akieleza kuwa hayupo katika nafasi ya kutoa msimamo wa menejimenti.
“Akitaka kuondoka ni yeye, mimi siwezi kuzungumza chochote, mwenyewe ndiye anajua nini anataka kukifanya, lakini siwezi kuweka msimamo wa uongozi,” amesema Bandari.