KMC chini ya Kocha Kally Ongala, imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pamba Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa leo Desemba 16, 2024 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Huo ni ushindi wa kwanza kwa Ongala tangu akabidhiwe kikosi hicho Novemba 14, 2024 akichukua nafasi ya Abdihamid Moallin aliyetimkia Yanga baada ya kushuhudia mechi tatu zilizopita kuambulia sare moja na vipigo viwili.
Bao la Hance Masoud dakika ya 88, lilitosha kuipa ushindi KMC ikiwa uwanja wa nyumbani na kufikisha pointi 18 ikitoka nafasi ya 11 na kusogea hadi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara huku Pamba Jiji ikiendelea kusalia nafasi ya 13 na pointi 12 ambapo timu zote zimekamilisha mzunguko wa kwanza kwa kucheza mechi 15.
Akizungumza baada ya mchezo huo kutamatika, Kocha wa Pamba Jiji, Fred Felix Minziro, alisema kama wangekuwa makini wangeimaliza mechi kipindi cha kwanza kutokana na nafasi walizotengeneza.
“Tuliikamata mechi vizuri kipindi cha kwanza lakini hatukuzitumia nafasi, baadhi ya nyota walioingia kama Habib Kyombo na Deus Kaseke bado ni mapema kuelezea viwango vyao ingawa tumejaribu kugusa kila idara kuhakikisha tunakuwa na kikosi imara,” amesema Minziro.
Kocha wa KMC, Kally Ongala alisema licha ya kuchukua pointi tatu lakini bado timu haijacheza vizuri akikiri wana safari ndefu.
“Nimefurahia pointi tatu lakini kwa kiwango cha timu sijaridhishwa, tumegawa nafasi nyingi kwa wapinzani wetu, bado safari ni ndefu katika kuhakikisha tunakuwa bora zaidi,” amesema Ongala.