Wadatooga ni kabila lenye mila za kushtua na kusisimua. Ikiwa kwenu mnalaani wizi, kwao ni fahari na heshima kubwa.
Kama haitoshi ukiwa unaiba ng’ombe au kugombania mwanamke kwao ndio ujasiri.
Yote haya ni kutokana na wao kuwa wafugaji, hivyo wakati mkulima analilia mazao yake kuharibika kutokana na ukame, Mtatooga analilia ng’ombe wake kukosa majani.
Mdatooga kwake nyumba si kipaumbele, na popote inaposhiba mifugo yake basi hapo ndiyo nyumbani.
Wakati Wasukuma wanasalimia kwa kuchuchumaa ikatafsiriwa ndiyo heshima, Mdatooga yeye atakupeleka zizini ili umpe heshima yake.
Utajiri kwao hupimwa kwa idadi kubwa ya ng’ombe, mbuzi na kondoo, na kama unaona hujaridhika na idadi ya mifugo yako, ni ruksa kumvamia mnyonge wako na kumpora ujazie zizi lako.
Kama hayo hayatoshi, sasa kutana na mkasa mwingine wa kushangaza kwa watu wa kabila la Wadatooga. Unajua kama kwao kung’oa jino ni kitu cha kawaida?
Iko hivi; wao hung’oa jino moja la chini ili waweze kupiga mluzi mithili ya filimbi na kupata sauti murua waliyoikusudia wachezapo ngoma zao za asili.
Kabila hili lenye asili ya Ethiopia, kwa sasa linapatikana kaskazini mwa Tanzania katika mikoa ya Manyara, Arusha, Singida na Mara. Kabila hili limekuwa na kawaida ya kuondoa jino hilo la chini mara baada ya meno ya utotoni kutoka na kuota meno mengine.
Sababu nyingine ya kabila hilo kuondoa jino la chini, ni pale anapochunga mifugo, uwepo wa nafasi ya chini iliyotolewa jino, husaidia sauti ya mluzi kufika mbali na kuzuia wanyama kufanya uharibifu wa mazao ya wakulima.
Hivi umeshakutana na watu wakiwa na alama ya duara ilichomwa na moto kwenye paji la uso? Hao ndiyo Wadatooga na mila zao, wengi huhisi ni aina ya urembo, lakini sivyo ilivyo.
Alama hii huitwa “Nundi” na ni tiba kwa wagonjwa wa kipanda uso. Pia huwekwa kwa kutumia kinyesi cha mbuzi au punje ya muhindi, iliyowekwa motoni ikiwa imechomekwa kwenye chuma chembamba mfano wa spoku na kupata moto. Kisha kipande cha punje hiyo hutolewa na kuwekwa kwenye paji la uso na katikati ya kichwa.
Aina hii ya tiba imeambatana na imani kuwa, maumivu hayo ya kipanda uso huja baada ya utosi kutokomaa, lakini pia mstari unaotenganisha vipande viwili vya fuvu kutofunga inavyotakiwa na hivyo kusababisha maumivu hayo.
Sambamba na hilo, sidhani kama utakuwa mgeni sana, wa zile imani za kijamii kuwa kuna watu wenye macho mabaya, ambapo huzaliwa hivyo na kuwa akitazama chakula kikiwa motoni kinapikwa, basi hakitaiva hata ukikoka moto mpaka kesho.
Katika kabila hili lenye asili ya kinailotiki,suala hili kwao si tatizo na aina hii ya watu hujulikana wakiwa bado hawajazaliwa kutokana na ishara mbalimbali zinazomtokea mama, baba au watu wa karibu na ukoo husika.
Matibabu ya kuondoa hali hiyo hufanyika kwa kuchanjwa katikati ya jicho na nyusi, huku wakifanya baadhi ya matambiko na kuweka dawa za mitishamba ambapo kwa imani zao huondoa nguvu hizo.
Baada ya kupata tiba hiyo, suala hilo hufikia tamati na hakutakuwa na madhara ya namna yoyote yatokanayo na mtu huyo kutazama kitu chochote.
Jambo la kushangaza kabila hili lina ndoa za aina tatu ambapo ndoa ya kwanza ni ile ya kutuma mshenga na kukubaliana na wazazi.
Ya pili ni ile ya kukubaliana na binti bila kushirikisha wazazi na ndoa ya tatu ni ile ndoa isiyo na ridhaa ya binti wala mzazi; kwa kifupi binti hutekwa.
Jambo jema ni kwamba kijana wa Kidatooga hufanya uamuzi wa kuoa baada ya kijana kumchunguza binti kwa muda wa kutosha, na kujua aina ya familia aliyotoka binti huyo.
Hapa huzingatia mambo makuu matatu, uchapaji kazi wa binti, kutokuwa na tetesi za uchawi katika familia na pia utajiri wa ng’ombe wa familia ya binti huyo.
Katika kabila hili, binti akipata mimba nje ya ndoa, hutengwa na jamiii nzima na kunyolewa kipara kisha kutelekezwa kwa bibi yeyote ambae hakuwahi kujaaliwa mtoto.
Damu kwao ni kinywaji kizuri kwa kabila hili, na mara nyingi hupata damu hii bila kuchinja ng’ombe. Mara nyingi huwapiga mshale kwenye mshipa wa shingo ya dume aliyenona na kuikinga tayari kwa kuchemshwa na kuliwa.
Hata hivyo, licha ya mikasa yao mingi ya kushangaza ambayo hapa tumeangazia baadhi tu, Watatooga wanasifika kwa kuwa wa kweli, wajasiri na wasiri.
Ni jamii inayozingatia nidhamu na heshima kwa waliowazidi, hupenda kujitenga na mara nyingi wanapenda amani wakati wote. Hata hivyo, wanapochokozwa huwa wakali kuliko simba jike mwenye njaa.