T-PESA YATAKIWA KUZINGATIA SHERIA ZA FEDHA NA UBUNIFU KATIKA UTOAJI HUDUMA

TTCL PESA LTD (T-PESA,) Kampuni Tanzu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) imehakikishiwa kupewa ushirikiano pamoja na mahitaji ya rasilimali na kutakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria za Fedha za ndani na nje ya Nchi na kuwa na ubunifu wa biashara na utendaji katika kutoa huduma za kidijitali ndani na nje ya Nchi.

Hayo yameeelezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) Zuhura Muro jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL PESA LTD (T-PESA,) pamoja na Bodi ya Wadhamini ya T-PESA na kuielekeza bodi hiyo kuwa na mtazamo mpana pamoja na ubunifu wa biashara na utendaji ili kuleta matokeo chanya katika Shirika hilo.

” Kazi hii inahitaji umakini, weledi na hekima kubwa ili kufikisha malengo na maono ya T-PESA….Mpango mkakati wa mwaka 2022/2026/27 unaotekelezwa utachochea mafanikio na kufanya mapinduzi makubwa ya teknolojia na uchumi wa kidijitali katika kutoa huduma za kifedha na malipo ndani na nje ya Nchi ….Tunakwenda Globally.” Amesema.

Amewaelekeza kuongeza ubunifu wa bidhaa pamoja na huduma zinazotolewa kwa wateja ili kukuza uchumi wa kidijitali, kutanua wigo wa kibiashara na kuongeza faida pamoja na hisa ili kutoa gawio kwa Serikali kwa mujibu wa maono ya Shirika hilo.

Amesema, Jukumu kubwa la Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL PESA na Bodi ya Wadhamini ni kuikuza kampuni hiyo tanzu na kuiweka katika misingi ya kupanua wigo wa shughuli zake ndani na nje ya nchi na kuifanya kuwa kiungo muhimu cha malipo ya kidijitali ndani ya Afrika na dunia nzima kwa kuwa biashara hiyo haina mipaka.

Aidha amewashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wa Shirika hilo kwa kuwa na utulivu na hamasa ya kufanya kazi kwa uzalendo.

Kwa upande Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) Mhandisi. Peter Ulanga amesema lengo kuu ni kuhakikisha Shirika kupitia kampuni Tanzu ya T-PESA inajiweka vizuri katika utoaji wa huduma za miamala ya simu ndani na nje ya Nchi.

” Tuna imani na Bodi hii mpya tutaweza kuongeza usikivu wa huduma zetu ndani na nje ya Nchi kwa kuwa T-PESA ina uwezo wa kutoa huduma za kifedha ndani na nje ya Nchi….Tunakwenda kidijitali.” Amesema.

Pia Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL PESA (T-PESA,) Richard Mayongela amesema bodi hiyo imejipanga kutimiza maono ya Shirika hilo kwa kutoa huduma bora za Fedha mtandao ndani ya nje ya mipaka ya Tanzania.

Mayongela amesema, ndani ya miaka mitano ijayo T-PESA itakuwa katika ramani nzuri ikiwemo kutoa huduma za kifedha kidijitali kimataifa na wameanza kuzungumza na wadau mbalimbali wakiwemo UDART na tayari wametengeneza kamati ya ukaguzi kwa utekelezaji zaidi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) Zuhura Muro akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL PESA na Bodi ya Wadhamini na kuwataka wajumbe hao kuzingatia ubunifu na sheria katika utekelezaji wa majukumu yao. Jijini Dar es Salaam.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL PESA LTD Richard Mayongela akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa wajipanga kutimiza malengo ya Shirika hilo kwa vitendo zaidi. Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) Mhandisi. Peter Ulanga akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa Wana imani na bodi hiyo mpya katika kuleta usikivu wa huduma zao ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Jijini Dar es Salaam.

Picha ya pamoja

Related Posts