Waziri Mkuu kuongoza majaribio SGR Dar-Dodoma Aprili 21

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuongoza safari ya majaribio ya treni ya reli ya kisasa (SGR) itakayofanya safari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ikiwa na watu takriban 600.

Majaribio hayo yatafanyika Aprili 21, 2024.  Katika treni hiyo Majaliwa ataambatana na viongozi wa Serikali, dini na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenda Dodoma kwa ibada maalumu Aprili 22, 2024 ya kuliombea Taifa na shughuli ya kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Aprili 19, 2024 na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhandisi Cyprian Luhemeja wakati akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla katika ufunguzi wa Maonyesho ya Biashara Miaka 60 ya Muungano, katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

“Treni ya kisasa itaanza kufanya kazi kwa kuwasafirisha viongozi wa dini kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma wananchi mjitokeze kwa wingi kushuhudia safari hiyo ya kihistoria,” amesema Luhemeja.

Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla akiwapungia wananchi waliofika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam kwa ajili ya ufunguzi wa Maonyesho ya Biashara Miaka 60 ya Muungano. Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Shirika la Reli Tanzania (TRC), Jamila Mbarouk amesema safari hiyo ni mwendelezo wa majaribio baada ya awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kufanikiwa.

Jamila amesema safari hiyo itajumuisha viongozi wote wa dini, Serikali na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Mabehewa yatakuwa mapya kila kitu kipya na tunataraji kutumia mabehewa kati ya manane hadi 10, maombi yatafanyika Aprili 22 uwanja wa Jamhuri Dodoma,” amesema Jamila akizungumza na Mwananchi.

Awamu ya kwanza ya majaribio ya treni hiyo yalifanyika Februari 26,2024 kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ikiwa na mabehewa manane ikitumia saa 2:20 kufika Morogoro.

Mabehewa sita ya ghorofa ya treni ya SGR yaliwasili nchini kwa mara ya kwanza Juni mwaka jana yakitokea nchini Ujerumani. Desemba mwaka jana pia TRC ikatangaza kupokea vichwa vipya vitatu vya treni za umeme na mabehewa mapya 27 ya abiria.

Aprili 3, 2024, TRC ilipokea seti ya kwanza ya treni ya kisasa ya Eletric Multiple Unit (EMU), vichwa vitano vya umeme na mabehewa matatu ya abiria.

Taarifa ya TRC iliyotolewa na Jamila ilisema Serikali ilifanya ununuzi wa seti 10, za treni ya kisasa zijulikanazo Eletric Multiple Unit kutoka kwa watengenezaji wa kampuni ya Hyundai Rotem ya nchini Korea ya Kusini.

“Seti moja ya EMU ina uwezo wa kubeba abiria 589 na kutembea kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa. EMU ni treni iliyoundwa kwa teknolojia ya kisasa inayowezesha abiria kupata huduma muhimu ikiwemo mtandao (Wi-Fi).

Sehemu za kukaa watu wenye mahitaji maalumu, mifumo ubaridi na kamera za usalama (CCTV Camera,” amesema 

Jamila amesema Serikali kupitia shirika hilo imepokea jumla ya mabehewa 65 ya abiria, vichwa 9 vya umeme na seti moja ya EMU. Seti zingine za EMU zitaendelea kuwasili kila mwezi hadi Oktoba mwaka huu.

Akifungua maonyesho  hayo, Abdulla amesema kutokana na muungano, uchumi umeimarika.
 
“Tumeshuhudia kuimarika kwa miundombinu hususani ya barabara na huduma za kijamii ikiwamo afya, maji na elimu, katika kuhakikisha usawa wa utoaji wa huduma kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano, hadi sasa taasisi 33  kati ya 39  za Muungano zilizopo Tanzania Bara zimefungua Ofisi Zanzibar,” amesema.

Abdulla amesema amani na umoja nchini utaletwa na muungano hivyo kama wapo watu wenye dukuduku kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar waziwasilishe serikalini na watasikilizwa.

Makamu huyo wa Rais amesema  katika kipindi cha miaka mitatu, 2021 hadi 2024 hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwepo kwenye muungano.

Amesema utatuzi wa changamoto za muungano umeongeza imani ya Watanzania kwa Serikali na hivyo kuimarisha, kudumisha amani ya muda mrefu.
 

Related Posts