Waasi wa M23 wauteka mji wa Alimbongo mashariki mwa Kongo – DW – 17.12.2024

Kulingana na vyanzo vya kijeshi na vya ndani ni kwamba jeshi la Kongo limepoteza udhibiti wa mji wa Alimbongo. Mji huo wa zaidi ya wakazi 20,000 ni kama kilomita 40 na mji wa kibiashara wa Butembo, ulioko Kaskazini mwa jimbo la Kivu-Kaskazini. Kutekwa kwa mji wa Alimbongo kumefuatia mapigano makali ya siku 16 baina ya jeshi la Kongo na waasi hao wa M23. Jumapili waasi wa M23 waliuteka mji mwingine wa Matembe ulioko yapata kilomita 10 na Alimbongo.

Afisa mmoja wa jeshi ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema wanajeshi wa Kongo walilazimika kuondoka baada ya mapigano makali dhidi ya waasi. Mji huo wa Alimbongo ulikuwa ngome kuu ya jeshi ili kuzuia waasi wa M23 kusonga mbele kwenye miji mikubwa ya Lubero, Butembo na Beni.

“Tumeshutumu kuzuka kwa vita”

Alain Kiwewa, mkuu wa mtaa wa Lubero, amesema mashambulizi katika maeneo hayo mawili yalisababisha mmiminiko wa watu waliokimbia mapigano kuelekea vijiji jirani. Taarifa hiyo imethibitishwa pia na mkuu wa asasi za kiraia jimboni Kivuya Kaskazini, John Banyene ameiambia DW kwamba wakimbizi hao wamekosa huduma za kibinamu.

“Wakaazi wengi wamekimbia na sasa hawana msaada wowote.Wengi wao wako katika dhiki ya kukosa msaada wa kibinadamu. Hali hiyo tumeishutumu. Na kilichotokea hivi sasa kinasabishwa na rais wa Rwanda kukataa kushiriki mkutano wa Luanda kwa ajili ya amani ya Kivu.”, alisema Banyene. 

Kongo na Rwanda zatupiana lawama

Maelfu ya raia wameyakimbia makaazi yao huko mashariki mwa Kongo kufuatia mapiganao ya hivi karibuni
Maelfu ya raia wameyakimbia makaazi yao huko mashariki mwa Kongo kufuatia mapiganao ya hivi karibuniPicha: Guerchom Ndebo/AFP/Getty Images

Ni kwa mara ya kwanza waasi wa M23 kuyateka maeneo hayo toka uasi wa kundi hilo mnamo mwaka 2012. Mapigano hayo yameshika kasi siku moja tu baada ya kuvunjika kwa mkutano uliopangwa baina marais Felix Tshisekedi wa Kongo na Paul Kagame wa Rwanda chini ya upatanishi wa Rais wa Angola.

Kongo na Rwanda zimetupiana lawama ya kutofanikishwa kwa mazungumzo hayo ambayo yalilenga kutia saini mkataba wa kumaliza vita. Kwenye mkutano na mabalozi wa nchi za nje mjini Kinshasa, Jumatatu (16.12.2024 ), waziri wa mambo ya nje wa Kongo, Therese Kayikwamba, alizitaka nchi hizo kufanya chaguo la kuiunga mkono Kongo au Rwanda katika mzozo uliopo hivi sasa. Kayikwamba amesema wadau wa Kongo ni lazima kuchukuwa hatua madhubuti dhidi ya Rwanda, maneno peke hayatoshi.

UPDF kuwalenga mamluki wazungu ?

Kwenye tukio jingine na lakusangaza, Mkuu wa jeshi la Uganda, Muhoozi Kainerugaba amewaonya mamluki wote wazungu walioko mashariki mwa Kongo kwamba ifikapo Januri 2 mwakani watashambuliwa na jeshi la Uganda UPDF, linaloendesha operesheni maalumu ya kijeshi dhidi ya waasi wa ADF, huko mashariki mwa Kongo.

Kwenye ujumbe aliochapisha kwenye mtandao wake wa X, Kainerugaba amesema kufikia desemba mwakani hakutokuweko tena na mamluki wa kizungu nchini Kongo.

Taarifa zinaelezea kuwa serikali ya Kongo iliwaajiri mamluki kadhaa kutoka mataifa ya Ulaya ili kuwatimua waasi wa M23 huko mashariki mwa Kongo.

Related Posts