VIDEO: Lissu apalia makaa kupambana na Mbowe Chadema, atoa kauli kuhama

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu amesema siyo ajabu kuwania uenyekiti wa chama hicho, na hana wasiwasi kupambana na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Kauli hiyo ya Lissu imekuja baada ya baadhi ya makada kukosoa hatua yake ya kuwania uenyekiti wa chama, ikizingatiwa awali aliwasilisha barua ya kugombea umakamu, lakini baadaye akabadili uamuzi huo.

Lissu ambaye baadaye leo  atachukua fomu ya kuwania kiti hicho, amesema kila inapofika uchaguzi mkuu wa chama hicho, makada wengi wamekuwa wakijitokeza kuchuana kama ilivyo demokrasia ya Chadema, lakini watu wanashangaa yeye kujitosa katika kinyang’anyiro hicho.

“Kitu ambacho wanakiona cha ajabu ni hiki, mara hii makamu mwenyekiti anagombea hii?. Sasa mlitaka achukue nani? Kama siyo makamu mwenyekiti, nani ameandikiwa kuchukua fomu (uenyekiti) na nani asichukue?,”.

“Kinachoonekana cha ajabu ni hicho tu, kwamba mara hii makamu mwenyekiti wa chama anagombea, lakini mwenyekiti mwenyewe (Freeman Mbowe) wala hajasema kama anagombea. Kelele zote hizi kwa sababu makamu mwenyekiti amesema anagombea, wakati mwenyekiti hajasema,” amesema Lissu.

Lissu ambaye ni mbunge wa zamani wa Singida Mashariki ameeleza hayo leo Jumanne Desemba 17, 2024 katika mahojiano ya kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Clouds Tv yaliyofanyika nyumbani kwake Tegeta Wilaya ya Kinondoni, jijini hapa.

Desemba 11, 2024 Lissu aliyewahi kuwa mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, alitangaza kuwania uenyekiti wa Chadema, akisema kwa mazingira ya sasa ya siasa, chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinamuhitaji kiongozi kama yeye.

Katika mahojiano hayo, Lissu amedai kuwa msingi wa kelele hizo kutokana na hatua yake ya kuwania uenyekiti kwa mujibu wa sheria na katiba ya Chadema hakuna.

“Sina wasiwasi wowote akigombea hata kidogo, sijawahi kuwa mwenyekiti. Nisipochaguliwa nitakuwa sijawahi kuwa mwenyekiti wa chama, nikichaguliwa nitakuwa mwenyekiti wa nne wa chama hiki,”amesema Lissu.


Lissu alivyojipanga kupambana na Mbowe

Lissu amesema hana ugomvi wala vita na Mbowe au viongozi wengi wakuu wa Chadema, ndiyo maana baada ya kutangaza nia ya kuwania uenyekiti, kesho waliketi pamoja kwenye kikao cha kamati kuu.

“Ipo wazi tuna tofautiana kimsimamo, kimtazamo wa mambo mengine, lakini kuna mengine mengi tunakubaliana, ndiyo maana tupo chama kimoja,”amesema Lissu.

Amesema yeye ni mwanamageuzi ametumia takribani miaka 20 katika kuijenga Chadema kwa jasho na damu na ataendelea kuwepo ndani ya chama hicho. Amesisitiza kuwa yeye ni mwanamageuzi awe na cheo au asiwe nacho.

“Nitabaki Chadema, mimi siyo mtu wa kutafuta malisho wala kufanya maagano, nitabaki kuwa mwanachama wa Chadema. Nisisitize tutafanya yale ambayo katiba ya chama imeelekeza, tufanye uchaguzi huru na haki, tusiwaingilie wapigakura,”amesema Lissu.

Lissu amesisitiza kuwa ikitokea ameshindwa uchaguzi kwa hila, basi atazisema na watu wazifahamu, akisema hila haiwezi kuondolewa bila kusemwa na kwamba ana matarajio mchakato huo utakuwa huru na haki.

“Katiba ya Chadema inasema chaguzi zinatakiwa ziwe huru na haki. Wanachama wanatakiwa wachague viongozi wao bila kuingiliwa au kudanganywa na kiongozi yeyote au mtawala, kama utafanyika udanganyifu au kuingiliwa kwa uchaguzi, haya sitayanyamazia hata kidogo,”amesema Lissu.

Katika mahojiano hayo pamoja na mambo mengine Lissu aliulizwa yeye ni injini au dereva, Lissu akajibu, “hili swali gumu kidogo. Nafikiri mimi ni ‘heavy duty mashine’ (mashine kubwa ya kufanya kazi).

Amesema yeye ni mpambanaji wakati wote, anavyojiona amezaliwa kwa ajili ya mapambano ya aina hiyo, hana mashaka yoyote kwamba akiwa hai hiyo ndiyo kazi yake, hatarajii kukimbia wala kuacha mapambano.

Pazia la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania nafasi mbalimbali za juu za chama hicho, limefunguliwa leo na litafungwa Januari 5,2025. Uchaguzi wa kuwapata viongozi wakuu wa Chadema utafanyika Januari 22,2025

Related Posts