Mcameroon Pamba amtaja Che Malone

NYOTA mpya wa Pamba Jiji, Cherif Ibrahim, ameweka wazi namna alivyovutiwa na kujiunga na klabu hiyo baada ya kumtaja beki wa Simba, Che Malone Fondoh kama chanzo cha kumshawishi kukubali ofa aliyopewa na miamba hiyo ya Mwanza.

Ibrahim ambaye amejiunga na Pamba Jiji kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo akitokea Coton Sport FC ya kwao Cameroon, amekiri kuwa mazungumzo na Che Malone, pamoja na mchezaji mwenzake kutoka taifa la Cameroon, Leonel Ateba ambao wote wanacheza Simba, yalimsaidia kufahamu vyema soka la Tanzania.

“Nilikuwa na mazungumzo na Che Malone na Leonel Ateba kuhusu ligi ya Tanzania. Che Malone aliniambia mambo mazuri sana kuhusu soka la hapa, akasisitiza ubora wa wachezaji na mazingira ya ligi. Alinifundisha kuhusu ushindani mkubwa wa Ligi Kuu Bara na kwamba ni fursa nzuri kwa mchezaji kama mimi, ambaye ninataka kuonyesha uwezo wangu,” alisema Ibrahim ambaye ni beki wa kushoto.

Kuhusu malengo yake msimu huu, Ibrahim alisema: “Mimi ni mchezaji ambaye ninapenda changamoto. Nimekuja hapa kutafuta mafanikio, nikiwa na malengo ya kuisaidia Pamba kufika mbali. Tutaendelea kujitahidi na mimi binafsi nitajituma ili niwe sehemu ya mafanikio ya timu,” alisema.

Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Fred Felix ‘Minziro’, ameonekana kuridhishwa na usajili wa Ibrahim, akimuelezea kama mchezaji mwenye kipaji kikubwa na uwezo wa kuleta mabadiliko katika timu.

“Cherif ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa, ana uwezo mkubwa wa kucheza nafasi mbalimbali uwanjani. Alipokuja kwetu, alileta ari na hamu ya kushinda. Hili ni jambo muhimu,” alisema.

Related Posts