Othman: Utitiri mifumo ya kodi unaua biashara Zanzibar

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud amesema kuna utitiri wa mifumo ya kodi ambao siyo tu unakatisha tamaa, bali unaua biashara Zanzibar.

Othman ametoa kauli hiyo leo Desemba 17, 2024 alipozungumza na ujumbe wa Tume ya Rais ya Kodi ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Balozi Ombeni Sefue.

Ujumbe huo ulifika Migombani, Unguja kujitambulisha na kupokea ushauri.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na kitengo cha habari cha ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, imeeleza Othman amesema ipo haja ya kuangaliwa mifumo hiyo, ili kuleta unafuu kwa wafanyabiashara na wananchi ambao wanaathirika na kodi hizo.

“Mfanyabiashara wa Zanzibar anajikuta anadaiwa kodi na mamlaka nyingi zikiwemo za Muungano na hizi za Zanzibar jambo linalodhoofisha biashara na kuleta usumbufu,” amesema.

Amesema ingetosha kwa mamlaka kuwekeza sehemu moja na kusimamia kazi hiyo kwa wafanyabiashara na wawekezaji ili kuleta wepesi wa utendaji, na siyo kila mmoja kumfikia na kumdai mfanyabiashara huyo-huyo.

“Zipo fursa nyingi katika sekta ya kilimo ila kutokana na ukali wa kodi wawekezaji wengi hulikwepa eneo hilo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa,” amesema.

Ameishauri tume kuwafikia wahusika na wananchi, kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wawekezaji ili kuleta ufanisi na kujenga ukaribu.

Pia kupunguza ukali wa kodi kwa masilahi ya uchumi wa nchi.

Balozi Sefue amesema wamepokea ushauri na watahakikisha wanaufanyia kazi. Amesema tume imeundwa baada ya kuona changamoto nyingi za kikodi.

Balozi Sefue amesema Rais Samia Suluhu Hassan alibaini changamoto nyingi katika eneo hilo, hivyo kuona haja ya kukusanywa mapendekezo yanayotekelezeka na kufanya mapitio na tathmini ya kina juu ya mazingira bora ya biashara ili kujenga ufanisi, kwa ajili ya kukuza pato la Taifa.

Oktoba 4, Rais Samia alizindua tume hiyo inayolenga kutathmini na kushauri kuhusu masuala ya kodi nchini, kujenga mfumo imara, thabiti na wa haki wa kikodi.

Related Posts