LICHA ya kupata ushindi wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji, lakini Kocha wa KMC, Kally Ongala amesema hajaridhika na kiwango cha timu yake huku akibainisha kuwa ushindi huo ni hatua muhimu katika ujenzi wa kikosi hicho.
Kocha huyo alikiri kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanyika ili kuhakikisha timu inafanikiwa zaidi.
Juzi Jumatatu, KMC iliichapa Pamba Jiji bao 1-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa KMC Complex, Dar ambapo ulikuwa ushindi wa kwanza kwa Ongala kwenye mechi nne za ligi alizoiongoza timu hiyo baada ya kukabidhiwa Novemba 14, mwaka huu.
“Huu ni ushindi muhimu, lakini hatuwezi kujivunia kwa kiwango cha sasa. Tunahitaji kuongeza bidii zaidi, hasa katika maeneo ya mwisho ya ushambuliaji,” alisema kocha huyo na kuongeza.
“Hii ni hatua, lakini tunahitaji kufika mbali zaidi. Tunajua matatizo yetu na tutayafanyia kazi.”
Ongala ambaye amerithi mikoba ya Abdihamid Moallin aliyetimkia Yanga, katika ligi alianza kibarua chake kwa kupoteza mechi dhidi ya Dodoma Jiji (2-1) na Tabora United (2-0), na kutoa suluhu dhidi ya Mashujaa kabla ya kuifunga Pamba Jiji. Pia alishinda mechi ya Kombe la FA raundi ya tatu kwa kuichapa Black Six mabao 5-0.
“Ushindi huu ni muhimu kwa kuongeza morali ya timu, lakini hatuwezi kuwa na furaha kwa kuona tunapata ushindi tu bila kuboresha,” alisema.
Kocha huyo ameendelea kulia na eneo la mwisho la ushambuliaji, akilalamika kuhusu kushindwa kutumia nafasi ambazo wamekuwa wakizitengeneza.
“Tunaendelea kuunda nafasi nyingi lakini hatufanikiwi kuzitumia. Hii ni changamoto kubwa kwetu. Kama hatutakuwa makini, tutapoteza mechi muhimu,” alibainisha.
Katika kuhakikisha mzunguko wa pili KMC inafanya vizuri, Ongala amesema atakitumia kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo kuboresha kikosi chake.
“Timu inacheza lakini inakosa mipango kwenye utengenezaji nafasi na kufunga wakati huohuo ukuta una mapungufu mengi na ndio sababu ya kuruhusu mabao.
“Mpango wangu ni kuhakikisha nasajili kwa kuzingatia mahitaji hii ni baada ya kukaa na timu na kubaini mapungufu eneo la ushambuliaji, kiungo na beki, ripoti nimeshakabidhi kwa viongozi na mchakato wa usajili umeanza,” alihitimisha Ongala huku akisisitiza kwamba endapo atafanikiwa kufanya maboresho kwenye maeneo hayo anaiona timu hiyo ikirudi kwenye ushindani.
KMC imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwa kushuka dimbani mara 15 ikikusanya pointi 18 baada ya kushinda michezo mitano, sare tatu na vipigo saba huku ikifunga mabao kumi na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 20.