Stone Town yaivuruga Vikapu | Mwanaspoti

Stone Town ya Zanzibar imeifunga Vikapu ya Kenya kwa pointi 52-16, katika fainali ya wachezaji wa umri wa miaka 18, iliyomalizika katika viwanja vya kituo cha michezo cha JMK Youth Park.

Mashindano hayo yanayojulikana kama JMK Basketball tournament, yalishirikisha   timu 50 kutoka Kenya, Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika mchezo huo, mchezaji Suleiman Khamisi wa Stone Town, alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa umri wa miaka 18.

Kwa upande wa umri wa miaka 18 wasichana, Vikapu ya Kenya iliishinda Nuglets  kwa pointi 26-22, huku Velentine Chilangati wa timu hiyo akiibuka mchezaji bora.

Kwa upande wa umri wa miaka 16 wavulana, Juhudi ilishinda Kigamboni kwa pointi 44-41, mchezaji bora akiibuka Steve Juma wa timu hiyo.

Vikapu iliifunga pia  Ukonga Queens kwa pointi 32-18, huku mchezaji bora wa mchezo huo akiwa ni Chelsea Adhiambo wa timu hiyo Vikapu.

Upande wa umri wa miaka 14 wavulana, Millenium kutoka Zanzibar iliifunga DB Oratory kwa pointi 27-11 na mchezaji bora alikuwa Abuu Bakar Juma  wa Millenium.

Kwa upande wa wasichana umri huo, Orkeeswa iliifunga Kigamboni kwa pointi 15-10 na mchezaji bora alikuwa Hekima Sa Itabau wa Orkeeswa.

Wakati huo huo Planet imeifunga Eagles kwa pointi 71-53, katika fainali ya kwanza ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Mwanza (MRBA) kwenye Uwanja wa Mirongo, mkoani humo.

Fainali hiyo inafanyika kwa timu hizo kucheza michezo mitatu ‘best of three play off’, huku fainali ya pili itakayochezwa, endapo Planet itashinda   itakuwa bingwa wa MRBA ,   kwa matokeo ya ushindi wa michezo 2-0.

Kama Eagles itashinda,   mchezo wa tatu utachezwa na mshindi atakayepatikana atakuwa bingwa kwa matokeo ya michezo 2-1.

Katika fainali ya kwanza iliyochezwa Planet iliongoza katika robo zote nne kwa pointi 12-7, 22-18, 18-10 na 19-18.

Kusekwa wa Planet alifunga pointi 19, aliongoza kwa kudaka mipira ya ‘rebound’ mara 10, huku kwa upande wa Eagles alikuwa Peter aliyefunga pointi 20.

Related Posts