Namungo matumaini yamerejea | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Namungo raia wa DR Congo, Fabrice Ngoy amesema ushindi wa mabao 3-2, dhidi ya KenGold, kwa kiasi kikubwa umewapa motisha ya kuendelea kupambana zaidi baada ya kuanza msimu vibaya.

Kauli ya nyota huyo alifunga bao moja katika ushindi huo, imekuja baada ya Namungo kucheza mechi 14 za ligi msimu huu ikishinda nne, sare moja na kupoteza tisa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ngoy ambaye hilo linakuwa bao lake la kwanza msimu huu katika Ligi Kuu Bara alisema, mbali na timu kurejea kwenye matumaini ya ushindani lakini pia bao alilofunga angalau kwa sasa limempa motisha ya kuendelea kupambana zaidi, huku akiweka wazi ataendelea kujituma akipewa nafasi ya kucheza.

“Msimu huu sijaanza vizuri kwa sababu ya majeraha ya hapa na pale lakini hata ukiangalia ushindani wa nafasi umekuwa ni mkubwa, bao nililofunga naamini limenisaidia kunijengea hali ya kujiamini na kurudisha imani kwa benchi letu la ufundi,” alisema Ngoy.

Nyota huyo alijiunga na Namungo msimu uliopita akitokea Tabora United baada ya kuonyesha uwezo mkubwa akiichezea Ligi ya Championship ambapo alifunga mabao 15 nyuma ya kinara, Edward Songo wa JKT Tanzania aliyefunga 18.

Msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, nyota huyo alifunga bao moja tu katika mchezo dhidi ya KMC uliomalizika kwa sare ya 1-1 Agosti 19, 2023, huku akitua nchini kwa mara ya kwanza msimu wa 2022-2023, akitokea Real Nakonde FC ya Zambia.

Kwa upande wa Kocha wa Namungo, Juma Mgunda alisema ushindi huo ni muhimu kwao baada ya kucheza michezo minne mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila ya ushindi tangu mara ya mwisho waliposhinda bao 1-0, dhidi ya Pamba Jiji Oktoba 28, mwaka huu.

“Wachezaji wote ni wazuri isipokuwa kuna mapungufu yanayojitokeza na tunaendelea kuyafanyia kazi lakini yapo mazuri pia ambayo nayo tunazidi kuhakikisha tunayaendeleza, ili tufanye vizuri kutokana na kufanya vibaya siku za hivi karibuni,” alisema Mgunda.

Naye nyota wa kikosi hicho, Hassan Kabunda, alisema: “Kikubwa tunaendelea kupambana kwa sababu tuna uwezo wa kufanya vizuri na ushindi dhidi ya KenGold umetuongezea kitu ingawa tuna kazi kubwa ya kufanya, tunaamini tutaendelea tulipoishia.”

Namungo iliyocheza mechi 14, keshokutwa Ijumaa itakuwa nyumbani kuikaribisha JKT Tanzania ukiwa ni mchezo wao wa mwisho mzunguko wa kwanza.

Related Posts