Changamoto ya soko yawasukuma wakulima kuanzisha kiwanda

Rombo. Wakulima wa ndizi zaidi ya 30 kutoka Kata ya Maharo, Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro, wameungana na kuanzisha kiwanda cha kuchakata ndizi ili kukabiliana na changamoto ya kukosekana kwa soko la uhakika la bidhaa hiyo.

Wakulima hao wamesema kukosekana kwa soko la uhakika kumewalazimu kuuza ndizi kwa bei ndogo, ambapo mkungu mmoja huuzwa kwa Sh2,000 hadi Sh5,000.

Wakulima hao wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti leo Jumanne Desemba 17, 2024, wamesema gharama za kutunza migomba hadi kufikia hatua ya kuvunwa ni kubwa ikilinganishwa na bei wanayouzia mazao yao sokoni.

Hata hivyo, wamesema kuanzishwa kwa kiwanda cha kuchakata ndizi kutatoa fursa ya kuzalisha bidhaa mbalimbali zitokanazo na zao hilo ukiwamo unga, hali itakayowapatia uhakika wa bei bora kwenye masoko.

Anna Mushi, mmoja wa wakulima wa ndizi wilayani humo, amesema kilo moja ya unga wa ndizi huuzwa kati ya Sh10,000 hadi Sh12,000, kinyume na bei ya mkungu mmoja wa ndizi.

“Fikiria, kuna wakati mkungu mmoja tunauza kati ya Sh2,000 hadi Sh3,000, lakini tukitengeneza unga au crips, faida inaweza kuwa zaidi ya Sh50,000, huu ni ubunifu mkubwa ambao utatuletea tija kwa wakulima,” amesema.

Naye Gabriel Kimario, mkulima mwingine wa ndizi amesema kuanzishwa kwa kiwanda hicho kutaleta manufaa makubwa na ufanisi kwa wakulima wa ndizi katika wilaya hiyo.

Naye, Mbunge wa  Rombo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameahidi kutafuta masoko ya uhakika kwa bidhaa za ndizi kutoka wilaya hiyo, ili wakulima waweze kupata tija.

“Tutalima ndizi na kuzipeleka Dubai, lakini ili tufanikiwe, lazima tufanye kilimo hiki kwa ushirika, ninaamini kufanya hivyo kutaleta manufaa makubwa,” amesema Profesa Mkenda.

Naye, Mwenyekiti wa kikundi cha Marsho, Bavon Asenga amesema kuwepo kwa kiwanda hicho, kutaleta manufaa makubwa kwa wakulima na kuongeza thamani ya zao la ndizi si kwa Rombo pekee bali Mko mzima wa Kilimanjaro.

Related Posts