Dar es Salaam. Wanahabari 10 waliokuwa wakifanya kazi katika Gazeti la Tanzania Daima lililokuwa linamilikiwa na Kampuni ya Fee Media Ltd, wameanza mchakato wa kumfunga gerezani mkurugenzi wa gazeti hilo, Dudley Mbowe kwa kukiuka makubaliano ya malipo ya madai ya stahiki zao.
Wanahabari hao, Maregesi Paul na wenzake tisa ambao walikuwa waandishi wa habari na wahariri wa gazeti hilo, wamefungua shauri la maombi ya utekelezaji dhidi ya Dudley ambaye ni mtoto wa mfanyabiashara na mwanasiasa maarufu wa siasa za upinzani nchini, Freeman Mbowe.
Mbali na Paul wanahabari wengine ambao ni waombaji katika shauri hilo ni Fidelis Felix, Christina Mwakangale, Janeth Josiah, Arodia Peter, Exuperius Kachenje, Hellen Sisy, Kulwa Mzee, Nora Damian na Makuburi Ally.
Katika shauri hilo wanahabari hao wanamtaka mdaiwa wao huyo ajieleze ni kwa nini asifungwe kama mfungwa wa madai kwa kushindwa kutekeleza amri na makubaliano ya malipo ya madai ya stahiki zao ambazo ni malimbikizo ya mishahara yao Sh62.7 milioni.
Shauri hilo limetajwa leo Desemba 17, 2024, mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mary Mrio. Ingawa mjibu maombi (mdaiwa huyo) alipewa hati ya wito wa kufika mahakamani, hata hivyo hakutokea.
Hivyo Naibu Msajili Mrio ameahirisha shauri hilo mpaka Januari 6, 2025, kwa ajili ya usikilizwaji.
Dudley alipotafutwa na Mwananchi kwa njia ya simu kuzungumzia shauri hilo na kutokufika kwake mahakamani, hakupokea simu badala yake alitaka atumiwe ujumbe.
Alipoulizwa kupitia ujumbe wa maneno kupitia WhatsApp hakujibu alichoulizwa kuhusu shauri hilo, badala yake alirejesha ujumbe wa salamu.
“Habari Magai, nategemea upo salama”, alijibu Dudley na hata aliporudishiwa ujumbe kumuuliza kutokufika kwake mahakamani hakujibu chochote.
Hii ni mara ya pili kwa wanahabari hao kufungua shauri la maombi ya utekelezaji amri ya malipo ya malimbikizo ya mishahara yao hiyo, iliyotolewa na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), kufuatia shauri la mgogoro wa kazi lililofunguliwa na wanahabari hao.
Wanahabari hao, walifungua shauri hilo CMA dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, baada mwajiri wao huyo kuvunja mikataba yao ya ajira kinyume cha sheria.
Katika shauri hilo la mgogoro wa kikazi namba 28461 la mwaka 2023, wanahabari hao walikuwa wakiomba kulipwa malimbikizo ya mishahara yao jumla ya Sh114 milioni.
Hata hivyo CMA katika uamuzi wake uliotolewa na Mwenyekiti Bonasia Mollel Julai 17 mwaka 2023, iliamuru wadai walipwe Sh62.7 milioni baada ya pande zote kukaa pamoja na kujadiliana na kufikia makubaliano.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu kila mwisho wa Oktoba, Desemba 30, 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa Februari, 2024.
Hata hivyo hakutekeleza ahadi hiyo na katika kutafuta ufumbuzi wa suala hilo, baadhi ya wanahabari hao kwa niaba ya wenzao Desemba 20 na 21, 2023 walikutana na kufanya majadiliano na Mbowe ambaye alichukua dhamana ya kuwalipa madeni yao mwishoni mwa Desemba.
Hata hivyo mpaka Februari Mbowe naye hakuwa amewatekeleza makubaliano hayo, hivyo wanahabari hao wakawasilisha mahakamani maombi ya utekelezaji wa tuzo hiyo.
Katika shauri la maombi hayo waliomba mahakama iamuru wakamate na kupiga mnada nyumba ya ghorofa moja iliyoko katika kiwanja namba 9, Mtaa wa Feza, barabara ya Chipata, Mikocheni A, waliyotaja kama moja ya mali za mdaiwa wao, Dudley.
Mahakama hiyo ilikubaliana na maombi hayo na Februari, 14, 2024 iliamuru nyumba hiyo ikamatwe, na nyumba hiyo ilikamatwa Februari 28, 2024 na dalali wa Mahakama, kampuni ya udalali ya MM Auctioneer & Debt Collector.
Hata hivyo nyumba hiyo iliachiliwa baada ya Mbowe kuweka pingamizi mahakamani kuwa nyumba hiyo si mali ya mdaiwa Dudley , bali ni mali yake na yeye si sehemu ya wadaiwa katika shauri hilo.
Kutokana hali hiyo wanahabari hao walitakiwa kutafuta mali nyingine inayomilikiwa na mdaiwa wao (Dudley) na kufungua tena shauri la maombi yao ya ukamataji mali kama sehemu ya utekelezaji wa tuzo yao.
Kwa mujibu wa wadai, baadaye Mbowe kupitia kwa wakili wake John Mallya aliomba kumalizana na wanahabari hao nje ya Mahakama ambapo wakapunguza kiasi cha madai yao na Mbowe aliahidi kuwalipa malipo ya awali Aprili na angemalizia malipo hayo Mei, 2024.
Hata hivyo wanadai kuwa mpaka sasa Mbowe hajatekeleza makubaliano hayo kama alivyowaahidi.
Kutokana na hali hivyo ndipo wamerudi mahakamani kufungua shauri la maombi ya utekelezaji dhidi ya Dudle, kwa kumtaka ajieleze kwa nini asikamatwe na kufungwa jela kama mfungwa wa madai kwa kushindwa kutekeleza amri ya kuwalipa madai yao.
Wakili wa Mbowe, Mallya hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo kwa kuwa simu yake ya mkono haikuwa hewani.