Wananchi walia na machimbo ya dhahabu, wataka yasitishwe

Chunya. Wananchi wa Kijiji cha Ifumbo, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, wameiomba Serikali kusitisha shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu ndani ya Mto Zira ili kulinda afya zao na mazingira dhidi ya uharibifu unaoendelea.

Aidha, wananchi hao wamesema maisha yao yako hatarini kutokana na kutegemea maji ya mto huo kwa matumizi ya kila siku.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne, Desemba 17, 2024, wakazi wa kijiji cha Ifumbo wamesema tangu mwaka 1977, walikuwa wakilitumia eneo la Mto Zira kwa shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu na kilimo kwa kuzingatia kanuni za utunzaji wa mazingira.

Akilizungumzia hilo, Michael Sanga (70) mkazi wa eneo hilo amesema wakati wananchi wakiendelea na shughuli za uchimbaji wa madini, Serikali ilisitisha shughuli hizo na badala yake kumpatia mwekezaji wa kampuni ya G&I Tech Trading Company Limited eneo hilo.

“Kimsingi hatuelewi maamuzi hayo ya Serikali kwani mwekezaji amefanya uharibifu mkubwa ndani ya Mto Zira kwa kuingiza mitambo na kuchimba bila kujali athari za kiafya kwa wananchi, wakati maji ya mto huo ni tegemeo kubwa kwa matumizi ya majumbani,” amesema Sanga.

Amesema changamoto hizo zimesababisha hasira miongoni mwa wananchi walioamua kuivamia kambi ya mwekezaji huyo na kufanya uharibifu, kwa lengo la kushinikiza Serikali kumuondoa na kusitisha shughuli za uchimbaji ndani ya mto huo.

“Wananchi hatuelewi hatma yetu baada ya Serikali kusitisha shughuli zetu za uchimbaji na badala yake kumpatia mwekezaji eneo lote kihalali. Sasa ni wakati wa viongozi kulitazama suala hili kwa upana wake ili kunusuru vijana wasijiingize kwenye uhalifu kwa kukosa maeneo ya utafutaji,” amesema Sanga.

Naye Ambokile Mwaitwalile amesema mgogoro kati ya wananchi na mwekezaji umeendelea kwa muda mrefu bila Serikali kuingilia kati, hali inayosababisha malumbano ya mara kwa mara.

Amesema Serikali inapaswa kuliona suala hilo kwa upana wake kwa kuwa tangu mwaka 1977 wananchi walikuwa wakitegemea eneo hilo kwa uchimbaji.

“Msimamo wetu tunaitaka Serikali ya wilaya iingilie kati suala hili. Endapo hatua hazitachukuliwa, tutachanga fedha kwenda kumuona waziri mwenye dhamana,” amesema  Mwaitwalile.

Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga ambaye ametolea ufafanuzi jambo hilo.

Amesema utaratibu wa uchimbaji wa dhahabu katika Mto Zira ni tofauti na maeneo mengine kwa kuwa mchimbaji lazima awe na kibali cha Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC).

“Hivi karibuni kuna watu walijiingiza kinyemela na kuanza uchimbaji bila kibali na kusababisha malalamiko kutoka kwa wenye leseni ambao wana hofu ya kufungiwa leseni zao kutokana na uharibifu huo,” amesema Batenga.

Na kuhusu mwekezaji wa kampuni ya G&I Tech Trading Company Limited mkuu huyo wa wilaya amesema anamiliki eneo hilo kihalali, kwa sababu ana vibali halali kutoka NEMC, huku akisema Mahakama iliamuru kuwaondoa waliokuwa wakichimba bila kibali.

“Suala la uchimbaji katika eneo hilo si leseni peke yake; lazima pia upate kibali maalumu kutoka NEMC. Nitawaita tena wataalamu wa NEMC waje kufanya tathmini ya eneo hilo,” amesema Batenga.

Kwa upande wake, mfanyabiashara na mmiliki wa kampuni ya G&I Tech Trading Company Limited, Seleman Kaniki amesema anamiliki eneo hilo kihalali kwa kuwa ana leseni na vibali kutoka mamlaka husika.

Kuhusu tuhuma za kufanya uharibifu wa mazingira, Kaniki amesema si sahihi kwani alishapatiwa baraka zote na NEMC baada ya kufanya tathmini ya kina ya mazingira ya eneo hilo.

“Nimezingatia taratibu zote za kisheria kwenye shughuli za uchimbaji, bila kusababisha athari za kimazingira. Tulishangazwa na kitendo cha wananchi kuja kufanya vurugu na uharibifu wa mali,” amesema Kaniki.

Related Posts