Dar es Salaam. Waswahili wanasema ukitupacho wewe kwa mwingine dhahabu na hii imedhihirika kwa wanachama tisa wa mradi wa uzalishaji funza wanaotumia mabaki ya chakula na maganda ya matunda kama ndizi na viazi kujiingizia kipato.
Wanachana hawo ambao ni wanufaika wa Mpango wa Maendeleo wa Kaya Maskini (Tasaf) walianza mradi wao mwaka 2021 baada ya kupewa mafunzo ya kujikwamua kiuchumi ikiwemo ufugaji funza.
Hayo yamesemwa na wanufaika wa Tasaf wakati wakitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wao kwa ujumbe wa Kamati ya Kudumu Baraza la Wawakilishi Zanzibar linalosimamia ofisi za viongozi wakuu wa kitaifa, waliofanya ziara kukagua utekelezaji wa mradi wa mpango wa kupunguza umasikini unaotekelezwa na Tasaf.
Wanakikundi hao wakiwa na eneo maalumu la kutekeleza shughuli zao, wamekuwa wakikusanya taka kutoka maeneo mbalimbali na kuziweka katika kizimba hicho ili kuvutia nzi chuma ambao hutaga mayai.
“Wiki mbili baadaye mayai haya hukua na kutengeneza funza ambao tunauza Sh3,000 kwa kilo na kadri taka zinavyokua nyingi ndiyo wingi wa funza tunaopata,” amesema Sina Said ambaye ni Katibu wa kikundi hicho.
Kupitia mradi huo wana uwezo wa kukusanya kati ya kilo tano hadi 10 kwa siku ambazo huuzwa kwa wafugaji wa samaki na kuku.
Mbali na funza hao pia maganda na mabaki ya chakula yanayotumika katika ufugaji huo baada ya kuoza huuzwa kama mbolea kwa wakulima wa mbogamboga kama mbolea za asili.
“Kiroba kimoja cha kilo 25 tunauza kwa kati ya Sh1,500 hadi Sh2,000 hivyo hakuna kitu tunachokitupa,” amesema.
Hata hivyo, baada ya watu kujua kuwa kikundi hicho kinatumia taka katika kujiingizia kipato walianza kuwauzia takataka jambo lililofanya upatikanaji wa malighafi kuwa wa kusuasua katika baadhi ya maeneo.
“Pia kunapokuwa na baridi, uzalishaji wa funza unapungua lakini kukiwa na joto ni msimu mzuri kuwazalisha. Na sasa tuko katika nafasi ya kutaka kutanua zaidi shughuli zetu kwa kutafuta masoko sehemu mbalimbali,” amesema.
Mtendaji wa Mtaa wa Mabwepande, Christina Ntanga amesema kwa sasa eneo lake lina kaya walengwa nane kutoka 59 zilizokuwapo kabla ya tathimini ya hali ya kiuchumi kufanyika na wengine kuondolewa.
“Tangu 2020 kaya walengwa 88 zimenufaika kwa kulipwa zaidi ya Sh58.1 milioni ambapo walitengeneza vikundi 10 vya kuweka na kukopa, huku wakijishughulisha na biashara ndogondogo na uzalishaji wa nzi chuma.
Kwa sasa kaya walengwa 58 wanajishughulisha na biashara ndogondogo kwa ajili ya kuimarisha uchumi wao,” amesema Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Tasaf, Tumpe Lukongo.
Amefafanua kuwa eneo hilo ni miongoni mwa waliochaguliwa kufanya mradi wa majaribio katika uzalishaji funza kupitia taka.
“Hii inadhihirisha kuwa tunaweza kufanya mradi huu katika manispaa nyingine zenye takataka ili waweze kusafisha makazi yanayozunguka mji na kujipatia faida,” amesema Lukongo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Machano Othman Said ameitaka halmashauri ya Kinondoni kukisaidia kikundi hicho kupata malighafi ili waweze kuzalisha funza hao kwa wingi.
“Nitamuambia mkurugenzi wawasaidie kupata taka ambazo ndiyo malighafi yenu kuu katika uzalishaji ili mkue zaidi. Hii ni kwa sababu taka mnazopewa mbali na kuwasaidia pia mnasaidia kusafisha mazingira,” amesema.
Hadi sasa kaya milioni 1.3 nchi nzima zinanufaika na mpango wa pili wa kupunguza umasikini unaotekelezwa na Tasaf ambao unatarajia kufikia ukomo Septemba mwakani.
Kupitia tathmini iliyofanywa miaka miwili iliyopita walibaini kaya 400,000 maisha yao yameboreka hivyo waliondolewa katika mpango.