Makonda apiga marufuku wafanyabiashara kuchangishwa kwa shughuli za Serikali

Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amepiga marufuku wafanyabiashara mkoani humo kuchangishwa michango kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiserikali.

Amesema wamekubaliana kwamba mkoani humo hakuna mfanyabiashara atakayepelekewa askari polisi au mgambo na kuwasumbua katika maeneo yao ya biashara.

Mkuu huyo wa mkoa amebainisha hayo leo Jumanne Disemba 17, 2024, mbele ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko wakati wa kongamano la 15 la wataalamu wa ununuzi na ugavi (PSPTB), jijini Arusha.

“Tumekubaliana hakuna mfanyabiashara kuchangishwa kwa ajili ya mambo ya Serikali, siyo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya au Mtendaji wa Kata, tunasema haya kwani jukumu letu ni kutengeneza mazingira mazuri ili hawa wafanyabiashara wafanye shughuli zao na walipe kodi,” amesema.

“Imekuwepo kasumba ya kila tukio ni michango, michango, mwisho wa siku inapoteza heshima ya kiongozi wa Serikali, inatweza utu wa Serikali, sisi kwenye mkoa wetu tumekataa,” Amesema.

Makonda amesema wamekataa tabia hiyo na kwa sasa wanaona faida, wafanyabiashara wenyewe wanafurahi kufanya jambo la Serikali.

Amesema wamekubaliana kwenye mkoa huo kwamba hakuna mfanyabiashara kupelekewa polisi au mgambo na kusumbuliwa katika eneo lake la biashara.

Amempongeza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuainisha utaratibu ambapo mkoani humo ikiwa kuna tatizo la kikodi kwa wafanyabiashara, mamlaka hiyo itazungumza na umoja uliopo chini ya wafanyabiashara husika,  ambao ni wanachama ili wachukue hatua.

“Maana yake tunaongeza wasaidizi wa kukusanya mapato bila bughudha na hilo linaleta tija sana na tumeona mafanikio na sasa hivi tunafanya kazi na Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato) baadaye tutaenda kwenye taasisi nyingine,” amesema.

Ameongeza kuwa wanaenda kufanya mfumo ambao ukiweza kufanya kazi vizuri wataomba usambae maeneo mengine kama ambavyo mtu akienda kituo cha mafuta kuweka mafuta, risiti anayopewa kodi inakatwa kwa mamlaka zote husika na kugawana ndani ya mfumo.

“Tunataka tufike hatua Arusha mfanyabiashara hakutani na Osha, Zimamoto wala nini, tozo zote zinakusanywa na mfumo mmoja halafu ndani ya Serikali zigawanywe kwa asilimia ambazo zimewekwa kwa mujibu wa sheria, hiyo itatuondolea mwanya wa rushwa na kuongeza wigo wa mapato na wananchi wafurahie Serikali,” ameongeza.

Related Posts