Watoto waliofariki kwa mlipuko wa gesi wazikwa, waombolezaji walani kuwafungia ndani

Moshi. Baadhi ya waombolezaji waliokuwepo kwenye maziko ya watoto wawili wa familia moja, waliofariki kwa kuungua moto baada ya mtungi wa gesi kulipuka wamelaani kitendo cha baadhi ya wazazi kuwaacha watoto wadogo ndani peke yao.

Watoto hao, Pendo (1) na Meshack Nyembo (3), wakazi wa kitongoji cha Darajani, mamlaka ya mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro walifariki Desemba 13, 2024 baada ya mtungi wa gesi waliokuwa wakiuchezea kulipuka.

Watoto hao walikuwa wamefungiwa ndani na mama yao ambaye alikwenda kwenye shughuli zake za utafutaji.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti, waombolezaji hao wamesema si sawa kuishi kwa uhasama na majirani lakini pia kufungia watoto ndani sio jambo jema linalopaswa kukemewa.

Jirani wa familia hiyo, Jane Mosha, amesema tukio hilo linapaswa kuwa somo kwa wazazi wote wenye tabia kama hiyo.

“Tunalaani vikali tabia ya kuwafungia watoto ndani. Wazazi tunapokuwa na ugomvi na majirani tusihusishe watoto, kwa sababu watoto hawana makosa. Wazazi tujifunze kutoka tukio hili,” amesema.

James Mboya, aliyeshiriki juhudi za uokoaji, amesema walifanikiwa kuvunja mlango na kumtoa mtoto wa kwanza, lakini walichelewa kumgundua wa pili ambaye tayari alikuwa ameungua vibaya.

“Tulivunja mlango na kumtoa mtoto wa kwanza tukampeleka hospitali, baadaye tukagundua wa pili naye yupo ndani. Moto ulikuwa mkubwa, lakini tulifanikiwa kuzima kwa maji,” amesema.

Balozi wa Mtaa wa Darajani, Semeni Mfinanga, ameetoa wito kwa wazazi kuacha tabia ya kuwafungia watoto ndani, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya majirani.

“Ni vibaya sana kufungia watoto ndani, hasa kama unakwenda mahali. Ni bora ukamwomba jirani akusaidie. Jirani yako ndiye ndugu yako wa karibu, tuishi kwa amani na upendo,” amesema.

Teobadi Chuwa, jirani mwingine, ameongeza kuwa Serikali inapaswa kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakumba wazazi, hasa wale wanaolazimika kuondoka nyumbani kwa ajili ya kazi.

“Hili tukio linatuumiza sana. Wazazi wanapaswa kuwa waangalifu zaidi. Kama mama hana muda wa kukaa na watoto, ni bora awaachie jirani au ndugu badala ya kuwafungia ndani,” amesema.

Awali Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi, alisema uchunguzi zaidi unafanyika kuhusu tukio hilo na taarifa kamili itatolewa baadaye.

Watoto hao walifariki dunia wakiwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Faraja iliyopo Himo baada ya kuungua moto,  wamezikwa katika makaburi ya Mieresini Himo.

Related Posts